Na. Farida Ramadhani na Joseph Mahumi, WF, Dodoma


Washirika wa Maendeleo nchini wameipongeza Serikali ya Tanzania kwa maendeleo mbalimbali hususan katika maeneo ya ukuaji wa uchumi, maendeleo ya rasilimali watu, mifumo ya chakula na miundombinu. 

Pongezi hizo zimetolewa jijini Dodoma katika Mkutano wa Majadiliano ya Kimkakati Ngazi ya Wataalamu kati ya Serikali (Makatibu Wakuu SMT na SMZ) na Washirika wa Maendeleo (Heads of Development Cooperation) ambayo yanalenga kujadili mbinu za kuongeza ustahimilivu wa kiuchumi na maendeleo jumuishi katika kipindi cha mabadiliko na changamoto za kiuchumia katika kipindi kisichotabirika.

Mwenyekiti Mwenza anayewakilisha Washirika wa Maendeleo, Bi. Sisan Ngongi Namondo alisema kuwa Tanzania imepiga hatua katika sekta za afya, miundombinu, na mageuzi ya sera, huku akibainisha maeneo matatu muhimu ambayo yatajadiliwa katika mkutanao huo kuwa ni utulivu wa uchumi wa taifa, ukuaji shirikishi, na uthabiti wa mabadiliko ya tabianchi. 

Bi. Namondo alisema kuwa Tanzania imeonyesha uimara mkubwa wa kiuchumi na usimamizi thabiti wa sera za fedha, lakini maendeleo ya haraka yanahitaji ushiriki mkubwa wa sekta binafsi, mageuzi ya kifedha, na mikakati madhubuti ya kupunguza umasikini.

Kwenye eneo la mabadiliko ya tabianchi na nishati, Mwenyekiti Mwenza huyo alisema kuwa juhudi za Tanzania kama vile Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia na Mkakati wa Nishati Jadidifu ni hatua muhimu, lakini uwekezaji zaidi unahitajika ili kuimarisha ujumuishaji wa nishati mbadala na kuongeza uthabiti wa mabadiliko ya tabianchi.

Bi. Sisan Ngongi Namondo aliahidi kuwa Washirka wa Maendeleo wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha nchi inapata maendeleo zaidi ya kiuchumi na kijamii.

Akizungumza wakati wa kufungua mkutano huo, kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Elmaamry Mwamba ambaye ni Mwenyekiti wa Mkutano huo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango -Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil, alisema mafanikio hayo yanatokana na kuimarika kwa ushirikiano kati ya Serikali na Washirika la Maendeleo.

Alisema katika maendeleo ya rasilimali watu, Serikali imeandaa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana (2007), ili kuendana na mabadiliko yanayoendelea ya kiuchumi, kiteknolojia, kisiasa na kijamii yanayotokea ndani na nje ya nchi. 

“Wizara yenye dhamana ya Maendeleo ya Vijana imeandaa Mkakati wa Utekelezaji wa Sera kwa kipindi cha miaka kumi (2024 – 2034) ikiwa ni nyenzo muhimu ya kufikia malengo yaliyoainishwa katika sera hiyo; inayolenga kukuza jamii ya vijana walio na ujuzi, ubunifu, ujuzi na uwezo wa kutumia teknolojia ipasavyo, waliowezeshwa na wanaolelewa ipasavyo, wazalendo, na wanaowajibika”, alibainisha Dkt. Akil..

Aliongeza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo (2014) ambayo inasisitiza ujumuishaji wa elimu ya ufundi na ufundi katika mfumo rasmi wa elimu na kukuza sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM) ili kukidhi mahitaji ya viwanda, na Sera ya Taifa ya Ajira (2008) ambayo inalenga katika kutengeneza ajira kwa vijana na kuboresha uwezo wa kuajiriwa kupitia mafunzo ya ufundi stadi na kuhamasisha uundaji wa ajira katika sekta binafsi.

Dkt. Akil alisisitiza juu ya uimarishaji wa mifumo ya chakula, Serikali imeboresha kilimo kupitia Teknolojia za Kilimo Hai (Climate-Smart Agriculture), ikiwemo matumizi ya mbegu zinazostahimili ukame, teknolojia za umwagiliaji pamoja na mradi wa Building a Better Tomorrow (BBT) ambao umewawezesha vijana kumiliki mashamba kwa kilimo cha kisasa.

“Juhudi hizi zinalenga kuongeza uzalishaji wa kilimo kupitia mbinu za kisasa za kilimo cha biashara, huku ikipunguza utegemezi wa mazao kutoka nje ya nchi na kukuza usalama wa chakula”, alisema Mwenyekiti, Dkt. Akil.

Kwenye suala la miundombinu, alisema Serikali imeendelea kuboresha miundombinu kupitia mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam na upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB), ambao sasa umeunganisha nchi saba jirani.

Naye, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Mursali Milanzi alisema katika mkutano huo, Tume imeelezea muelekeo wa Dira mpya ya maendeleo kwa kuwa sasa wapo katika hatua za mwisho za kutekeleza dira iliyopo.

Alisema pia wameelezea kuhusu miradi ya kipaumbele ambayo itatekelezwa kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na  Washirika mbalimbali wa Maendeleo kutoka nchi mbalimbali, Asasi zisizo za Kiserikali, pamoja na viongozi waandamizi wa Serikali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Share To:

Post A Comment: