Na Denis Chambi , Tanga.

SERIKALI imeanza  mchakato wa uboreshaji wa miundombinu ya Bomba la Tazama  linalosafirisha mafuta kutoka Tanzania hadi Zambia lengo likiwa ni kuongeza nchi zinazotumia huduma hiyo kutoka nchi 12 kwa sasa  hadi 14.

Hayo yameelezwa  February 17, 2025 na Naibu waziri Mkuu ambaye pia ni waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko wakati akifungua  kikao cha 4 cha Baraza la wafanyakazi wa Mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na maji " EWURA" Kilichofanyika Mkoani Tanga ambapo amesema kuwa uhitaji wa mafuta hapa nchini umeongezeka tofauti na awali.
 
Dkt. Biteko amesema kuwa Bomba hilo lililojengwa mwaka 1970  likiwa linatembea zaidi ya Kilomita 1,700 limekuwa halina vituo vya kushushia mafuta kwa muda mrefu na kupelekea msongamano wa magari katika bandari ya Dar es salaam hivyo Serikali imeamua pamoja na maboresho yatakayofanyika kujenga vituo mbalimbali hapa nchini.

Alisema moja wapo ya maeneo ambayo yatajengwa vituo hivyo ni Makambako Mkoani Mbeya pamoja na Morogoro ambapo vitarahisisha  usafirishaji wa Nishati hiyo pamoja na kuondoa mianya ya rushwa huku akibinisha kuwa bado Serikali inaendelea kufanya mazungumzo na Uganda kupitia mradi wa EACOP.

"Leo nishati Duniani ni  hitaji kubwa sasa hivi tuna bomba letu la Tazama linalopeleka mafuta Zambia limejengwa miaka ya 1970 mahitaji ya mafuta Zambia na sisi ndani  yamekuwa makubwa tunataka kulipanua kulitoa kwenye nchi 12 zilizopo hadi 14 tusingependa kuwa na Bomba ambalo linatembea zaidi ya Kilomita 1,700 bila ya kuwa na matank njiani" 

"Nia yetu ni kwamba tuondoe foleni  ya magari Dar es salaam yanayokuja kuchukua mafuta bandarini na kutengeneza msongamano tunataka mafuta ya Mbeya yachukuliwe Makambako na Morogoro bado tuna mazungumzo na watu wa Uganda 

Awali akizungumza mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi na  Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya udhibiti wa huduma za Nishati na maji 'EWURA' Dkt. James Andelile  alisema kuwa wameendelea kuhamasisha uwekezaji wa Nishati kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje.

"EWURA imejenga mazingira wezeshi kwaajili ya uwekezaji hapa nchini kwa viwango vya ufanisi kuanzia November hadi December 2024 tumetoa vibali 8 na  wawekezaji takribani hamsini ambao wameonyesha nia ya kuwekeza wakishamalizana na TPDC tutatoa vibali kwa wakati" alisema Dkt Andelile 

Alisema EWURA imetekeleza maagizo ya kufikisha huduma ya Nishati ya mafuta mpaka vijijini iliyotolewa na Dkt Biteko ambapo imeweza kupunguza gharama za vibali kutoka shilingi  laki Tano '500,000' hadi elfu hamsini '50,000'  pamoja na kupunguza maombi ya leseni kutoka Milioni moja '1,000,000' hadi shilingi  laki moja '100,000'.

"Agizo ambalo ulilitoa la kuwezesha ujenzi wa vituo  vya kuuza mafuta  katika maeneo ya vijiji mbalimbali na kupunguza masharti ya ujenzi wa mafuta ikiwemo kupunguza gharama za vibali kutoka laki Tano hadi shilingi elfu hamsini na kupunguza maombi ya leseni  kutoka Milioni moja mpaka laki moja tumeendelea kufanya mawasiliano na REA ili kuhakikisha vituo vingi vinajengwa vijijini na kurahisisha upatikanaji wa Nishati safi katika hali ya usalama" alisema.

Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batilda Buriani alisema kuwa Serikali imetoa kiasi cha  shilingi  Trillion  3.60 kwaajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya  usambazaji wa umeme ambapo tayari vijiji 763 vimefikiwa na huduma hiyo  pamoja na vitongoji 4,596 ikiwa ni sawa na asilimia 50.

" Sisi katika Mkoa wetu wa Tanga tumepata kiasi cha shilingi Trillion 3.60 ambazo zimeelekezwa katika miradi mbalimbali na tumefanikiwa kupeleka umeme  katika vijiji vyote 763 na kasi ya kupeleka umeme katika vitongoji vyetu 4,596 si kazi kubwa sana lengo ni kuhakikisha tunavifikia vitongoji vyote.

Alisema katika kutokomeza matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia  kwenye matumizi ya Nishati safi  Mkoa umeendelea kuzisimamia taasisi zenye watu zaidi ya 100 ikiwa ni maelekezo ya Serikali ambapo mpaka sasa taasisi 1493 zimeshakaguliwa huku wananchi zaidi ya 735,372 kati ya 2,600,000 wanatumia Nishati safi na salama. 

Share To:

Post A Comment: