Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini Ummy Mwalimu, amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuleta maendeleo katika Jiji la Tanga na Tanzania kwa ujumla.

Akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa CCM Mkwakwani leo Ijumaa Februari 28, 2025 ambapo Rais Samia ni mgeni rasmi, Ummy Mwalimu amewahakikishia wakazi wa Tanga kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Samia inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ambayo imeleta mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali.

Katika sekta ya elimu, Rais Samia amewezesha ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari, pamoja na madarasa mapya, ununuzi wa madawati, na kuendeleza sera ya elimu bila malipo.

 Pia, sekta ya afya imeimarishwa kwa kujengwa kwa vituo vya afya, zahanati, na kuboresha hospitali ya Rufaa ya Bombo na hospitali ya Wilaya ya Masiwani.

Mbunge huyo wa Tanga Mjini ameeleza kuwa, kwa upande wa miundombinu, Tanga sasa inapendeza kwa barabara za lami, taa za barabarani, na maboresho ya mifereji. Mradi wa barabara ya Tanga hadi Pangani umepewa kipaumbele, ambapo mkandarasi amelipwa Shilingi bilioni 10 ili kukamilisha ujenzi wake.

Katika sekta ya maji, Ummy amesema, Rais Samia amefanikisha upatikanaji wa maji safi kwa kata mbalimbali za Tanga kupitia mpango wa ‘Kijani Bond,’ ambao umetengewa zaidi ya Shilingi bilioni 54.

"Rais Samia ameleta mageuzi makubwa katika bandari ya Tanga kwa kuwekeza Shilingi bilioni 249.1, hatua ambayo imewezesha kupokea meli kubwa, kuongeza fursa za ajira, na kuchochea biashara. Pia, ujenzi wa masoko mapya kama soko la Makorora, soko la samaki Deep Sea, na soko la Mgandini umeendelea kuimarisha uchumi wa wananchi." alisema Ummy 

Mbunge Ummy amewasilisha maombi ya wakazi wa Tanga kwa Rais Samia, ikiwa ni pamoja na kufufua viwanda vya chuma, mbolea, saruji, na nguo ili kuongeza ajira kwa vijana na wananchi kwa ujumla. 

Pia, ameomba ujenzi wa chuo kikuu katika Jiji la Tanga na kupendekeza kiitwe Chuo Kikuu cha Shaaban Robert ili kuheshimu mchango wa mwanazuoni huyo.

Katika hitimisho lake, Ummy Mwalimu amemhakikishia Rais Samia kuwa wananchi wa Tanga Mjini wana imani naye na wako tayari kumpa kura zote mwezi Oktoba 2025 ili aendelee kuiongoza Tanzania na kuleta maendeleo zaidi.

















Share To:

Post A Comment: