Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeendelea kuonesha mchango wake mkubwa katika sekta ya mifugo kwa kuanzisha mradi wa utafiti wa NANO COMM, unaolenga kutengeneza tiba mbadala ya homa ya kiwele kwa wanyama wanaotoa maziwa. Kupitia utafiti huu, SUA inalenga kutatua changamoto sugu inayowakabili wafugaji wengi nchini, hususan katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Arusha, na Tanga.


Prof. Gaymary Bakari, Mhadhiri wa SUA na Mtafiti Kiongozi wa Mradi, amesema kuwa utafiti huu ni moja ya juhudi za chuo hicho katika kutafuta suluhisho la changamoto za wafugaji kupitia sayansi na tafiti

"Tumebaini kuwa homa ya kiwele imekuwa tatizo sugu kwa wafugaji wa wanyama wa maziwa, na wengi wao wanakosa tiba sahihi au wanatumia gharama kubwa kutibu mifugo yao," amesema Prof. Bakari.

Prof. Gaymary amesema kuwa matarajio ya mradi huo ni kuleta suluhisho la moja kwa moja kwa wafugaji, kusaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa, kupunguza gharama za matibabu, na kuimarisha uchumi wa wafugaji.

Ameongeza kuwa kwa miaka mingi, SUA imekuwa kinara wa tafiti mbalimbali zinazolenga kuboresha afya ya mifugo na uzalishaji wa mazao yake.

Aidha, Prof. Gaymary Bakari ameomba jamii kutoa ushirikiano wa karibu kwa mradi huu ili kufanikisha malengo yake huku akisisitiza kuwa ushirikiano wa jamii, hususan wafugaji na wadau wa mifugo, utakuwa muhimu katika kuhakikisha kuwa tiba zinazopatikana zinakuwa sahihi na zinafanikiwa kutatua changamoto za kiwelea katika sekta ya mifugo.

"Tutahitaji msaada wa wafugaji na jamii kwa ujumla ili tuweze kupata suluhisho bora litakalosaidia sekta hii kubwa na muhimu," amesema Prof. Bakari.

Ezekia Mbawa na Lisa Kisanga, ni wanafunzi wa Shahada ya Uzamili SUA, ambao ni watafiti washiriki katika mradi huu. Wameeleza kuwa mbali na kushiriki katika utafiti, mradi huo umewasomesha katika shahada zao za uzamili, jambo lililowapa fursa ya kupata ujuzi wa kina kuhusu tiba za mifugo na tafiti za kimataifa.

"Tunaamini kuwa kupitia utafiti huu, SUA itaendelea kuwa chombo muhimu cha mabadiliko chanya katika sekta ya mifugo nchini," amesema Mbalwa.



Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: