Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mheshimiwa Jerry William
Silaa (Mb), amesema Usalama wa Mitandao ya simu za mkononi na Intaneti
utaongeza imani kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano na hivyo
kuchagiza shughuli mbalimbali za uchumi wa kidijiti zinazohitaji mitandao
salama.
Waziri Silaa ameyasema hayo wakati akizindua Kampeni ya Usalama
Mtandaoni yenye jina “SITAPELIKI” wakati wa Kikao Kazi cha Wizara na
Wadau wa Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kilichofanyika katika
Ukumbi wa Mikutano Jengo la PAPU, jijini Arusha.
Aidha, Waziri Silaa aliongeza kuwa uzinduzi huu unalenga kukabiliana na
uhalifu kwenye mitandao ya Simu za Mkononi na Intaneti na kuwakumbusha watumiaji wa huduma za mawasiliano kuzingatia tahadhari
na elimu inayotolewa kuhusu matumizi sahihi na salama ya mitandao.
Kampeni ya uhamasishaji umma na watumiaji wa huduma za mawasiliano
kuhusu njia za kuwa salama mitandaoni na kuepuka ulaghai/utapeli yenye
jina la “SITAPELIKI”, inaendeshwa na Serikali kwa kushirikiana na watoa
huduma za Mawasiliano, na wadau wengine.
Amesema kuwa, Ulaghai na hatimaye wizi, hufanyika kwa matapeli kupiga
simu kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano na kutuma ujumbe mfupi, na
kuwataka watoe taarifa zao zinazohusu akaunti za pesa mtandao, au za
kibenki, miamala, nywila (neno la siri).
Utapeli mwingine ni pamoja na ulaghai kwenye mitandao ya kijamii (WhatsApp) kwa kuwashawishi watumiaji kubofya viunganishi (links)
vilivyotumwa kama ujumbe au kujibu ujumbe unaohusiana na fursa za kupata pesa za bure, ajira nakadhalika na matokeo yake taarifa za mhusika
kudukuliwa na kusababisha matatizo mengine.
Vilevile, Waziri Silaa alisema kuwa Huduma za Mawasiliano nchini zimeenea
sana na zinachangia na kurahisisha shughuli mbali mbali za kijamii na za
kiuchumi, hivyo Serikali haitavumilia wachache wanaotaka kuleta hofu na
kuondoa imani ya matumizi ya huduma za Mawasiliano”.
“Ulaghai mitandaoni unahujumu mikakati ya Serikali kuendeleza
ushirikishwaji wa wananchi kwenye mifumo ya kifedha na kujenga uchumi wa
kidijiti”, aliongeza.
Usalama na uimara wa mitandao unachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa watumiaji wa huduma mbalimbali za mawasiliano
zikiwemo huduma za kifedha kupitia simu za mkononi.
Waziri Silaa alitambua mchango wa wadau mbali mbali katika kukabiliana na
masuala ya utapeli/ulaghai mtandaoni na kutoa rai kama ifuatavyo:-
a) TCRA kuendelea kuimarisha usimamizi wa usalama na uimara wa
mitandao;
b) Watoa huduma kutoka katika Makampuni ya simu kuendelea kubuni
mbinu mbalimbali za utoaji wa elimu kuhusu usalama mtandaoni na
kuwafikia watumiaji wote, pamoja na kuwa na utaratibu maalum wa
kushughulikia masuala ya utapeli/ulaghai mtandaoni kwa uharaka pindi
wanapopokea malalamiko kutoka kwa wateja.
c) Vyombo vya Habari kuendelea kushirikiana katika kufikisha ujumbe huu
na kuhamasisha jamii yetu kutumia mtandao kwa usahihi na usalama
ili waweze kunufaika kikamilifu na fursa zilizopo mtandaoni.
d) Wadau wengine wote wanaohusika kwa namna moja au nyingine
kuhakikisha kuwa wanakuwa mstari wa mbele kushughulikia ipasavyo
masuala ya utapeli/ulaghai mtandaoni pindi wanapopokea malalamiko
kutoka kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano.
Post A Comment: