NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

TANZANIA inatarajiwa kuwa mwenyeji katika Mkutano wa 19 wa mwaka wa Jukwaa la Korosho Afrika ambao kufanyika Novemba 18 hadi 22, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo umendaliwa na Jukwaa la Korosho Afrika (ACA) kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho Tanzania na Umoja wa Wabanguaji Wakubwa wa Korosho Tanzania (TACP).

Pia Mkutano wa 19 wa Mwaka wa ACA unakusudiwa kuhudhuriwa na washiriki wasiopungua 500 kutoka nchi zote Duniani zikiwemo nchi 33 zinazolima korosho.

Baadhi ya nchi hizo ni pamoja na Ivory Coast, Cambodia, India, Vietnam, Brazil, Indonesia, Sri Lanka, Nigeria, Guinea Bissau, Burkina Faso, Mali, Benin, Ghana, Madagascar, Zambia, Msumbiji, Kenya, Mauritius, Visiwa vya Komoro na wenyeji Tanzania.

Akizungumza na Waandishi wa habari Januari 31, 2025 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Korosho Tanzania , Francis Alfred amesema Mkutano huo unakusudia kutangaza fursa za uwekezaji zilizoko kwenye tasnia ya Korosho kuanzia shambani ambapo wanategemea kupata uwekezaji kwenye mashamba makubwa ya korosho, kuongeza ubanguaji ambapo matarajio ni kuongezeka kwa viwanda vya kubangua na kusindika korosho na bidhaa zake na kuimarika kwa masoko kwa kufungua masoko ya korosho na bidhaa zake ndani na nje ya nchi za Afrika.

"Kwa upekee Mkutano huu utatumika kuhamasisha matumizi ya korosho na bidhaa zake kama vile mafuta ya ganda la korosho (Cashewnut Shell Liquid - CNSL), sharubati (juice), maziwa ya korosho (cashew milk), mvinyo (wine), nyama ya mabibo (cashew apple meat) na pombe kali. Aidha bidhaa nyingine kama ethanol zinaweza kutumika kwenye maabara za hospitali na shule zetu na hivyo kupanua wigo wa soko la korosho". Amesema Alfred.

Amesema mkutano huo utashirikisha wadau mbalimbali kutoka nchi ambazo ni walaji wa korosho ikiwa ni pamoja na Marekani, Nchi za Ulaya, China, Uarabuni, Mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini na nchi zingine za bara la Afrika.

Aidha amesema Serikali imefanya juhudi kubwa za kuendeleza zao la korosho ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu sasa imekuwa ikitoa pembejeo za korosho kwa wakulima kwa ruzuku ya 100%.

"Kwa mfano katika msimu wa 2024/2025 ruzuku ya pembejeo ilikuwa shilingi billioni 182. Utoaji wa pembejeo za ruzuku umechagiza kuongezeka kwa uzalishaji kutoka tani 310,000 msimu wa 2023/2024 hadi kufikia tani 410,000 kwa msimu wa 2024/2025 zilizouzwa kupitia minada". Amesema

Pamoja na hayo amesema ukusanyaji wa taarifa za uzalishaji unaendelea kwa kukusanya takwimu za korosho zinazobanguliwa majumbani kwenye vikundi vidogo na watu binafsi pamoja na uzalishaji katika mikoa mipya.

Amesema hadi mwisho wa msimu makadirio ni kuzalisha jumla ya tani 500,000 katika msimu wa 2024/2025.

"Bei ya korosho ghafi katika msimu wa 2024/2025 iliimarika na kufikia shilingi 4,195 kwa kilo ikiwa ni bei ya juu kuliko bei zote zilizopatikana kutoka nchi yetu ipate uhuru.". Ameeleza Alfred.

Hata hivyo amesema pamoja na uwepo wa mahitaji makubwa ya korosho ghafi katika soko la dunia, uamuzi wa Serikali kutumia mfumo wa mauzo wa Soko la Bidhaa (TMX) umesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ushindani katika minada na kuchangia katika kuimarika kwa bei.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ACA, Ernest Mintah amesema Mkutano huo unatarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 400 kutoka nchi mbalimbali duniani ambapo hii itakuwa mara ya tatu kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huukwani mara ya kwanza kwa kipindi cha miaka sita, baada ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo mwaka 2008 na 2019.

Amesema Mkutano wa ACA umekuwa ukijikita kwenye mada kuu inayoundwa kupitia mchakato wa kina ili kuakisi hali halisi na kushughulikia changamoto kuu zinazoikabili sekta ya karanga duniani ambapo katika Mkutano huu itajikita zaidi na kauli mbiu ya "Kufungua Fursa za Uwekezaji katika Karanga kwa Ukuaji Endelevu wa Uchumi."

"Mkutano wa mwaka huu utaangazia hitaji muhimu la kuwekeza kimkakati katika maeneo kama vile utafiti, maendeleo ya uwezo wa binadamu, miongozo ya sera, ubunifu na teknolojia, ufuatiliaji, usalama wa chakula, na mengineyo katika sekta ya karanga ili kuhamasisha ukuaji endelevu". Amesema Mintah.

Nae Mwenyekiti wa Umoja wa wabanguaji wa Korosho, Bahati Mayoma amesema ili kuweza kushiriki kwenye mkutano wa 19 wa mwaka wa ACA kila mshiriki atatakiwa kulipia kiasi cha shilingi 400,000 kwa watakaojisajili na kulipia kabla ya tarehe 15 Oktoba 2025 na shilingi 500,000 kwa watakaojisajili na kulipia baada ya tarehe 15 Oktoba 2025 kwa watanzania .

Aidha kwa wageni amesema itakuwa nia dola za Marekani 500 kwa wanachama wa ACA na dola za Marekani 700 kwa wasio wanachama wa ACA kwa watakaojisajili na na kulipia kabla ya tarehe 13 Agosti 2025 na dola za Marekani 700 kwa wanachama wa ACA na dola za Marekani 1,000 kwa wasio wanachama wa ACA kwa wakakaojisajili na kulipia baada ya tarehe 31 Agosti 2025.
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: