Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam


Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amekutana na kufanya majadiliano na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Profesa Palamagamba Kabudi, kuhusu maendeleo na changamoto zinazoikabili sekta ya michezo hususan mpira wa miguu nchini, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam.

Katika majadiliano hayo, Serikali imeipongeza TFF na Bodi yake ya Ligi, kwa kusimamia kwa weledi masuala ya maendeleo ya soka na kuliletea Taifa heshima kubwa barani Afrika na kupewa jukumu la kuandaa mashindano ya CHAN na AFCON, na kukubaliana pia namna tasinia ya utamaduni, sanaa na michezo  inavyoweza kutumika kuhamasisha uzalendo wa kulipa kodi kwa hiari, kupitia kampeni ya kudai na kutoa risiti kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania-TFF, Bw. Wallace Karia, amekubali mapendekezo ya Serikali na kuahidi kuwa suala la ulipaji kodi ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa na kuahidi kuwa watalichukulia kwa uzito suala hilo katika michezo yote ya mpira wa miguu inayosimamia na Taasisi hiyo.

Majadiliano hayo yaliwashirikisha viongozi wa juu wa Wizara ya Fedha, akiwemo Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Bw.Yusuph Mwenda, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania- TFF, Bw. Wallace Karia, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Bw.. Almas Kasongo, viongozi waandamizi wa Wizara ya Fedha, pamoja na Taasisi zinazosimamia michezo nchini.
Share To:

Post A Comment: