Na. Josephine Majura WF- Dodoma
Serikali imeeleza kuwa masaa yanayotumiwa na Wabunge wenye sifa ya Mhasibu wa Umma aliyeidhinishwa (CPA), katika ushiriki wa vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Mitaji ya Umma (PIC) pamoja na uchambuzi wa Bajeti ya Serikali yanatambuliwa kama ni mafunzo endelevu (CPD hours).
.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kilindi, Mhe. Omari Mohamed Kigua, alietaka kujua wakati ambao wabunge wenye sifa ya CPA Ushiriki wao kwenye Kamati za LAAC, PIC, PAC na Bajeti utachukuliwa kama CPE hours.
Alisema mafunzo endelevu rasmi (yaani uso kwa uso, au ya kielectroniki) na mafunzo endelevu yasiyo rasmi ikiwa ni pamoja na kushiriki mikutano ya kiufundi katika tasnia ya Uhasibu na Ukaguzi yanatambulika katika Mwongozo wa Mafunzo Endelevu ya Kihasibu Tanzania (Continued Professional Development- CPD Guideline), ulioidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya NBAA na kuanza kutumika rasmi Julai 01, 2020.
“Kwa kufuata mwongozo huo, na kwa kuzingatia muda unaotumiwa na Waheshimiwa wabunge wakati wa ushiriki wa mikutano ya Kamati za Bunge, hasa zile zinazohusu masuala ya uhasibu au ukaguzi kama LAAC, PIC, PAC na uchambuzi wa Bajeti ya Serikali, masaa wanayotumia wabunge wenye CPA yanatambuliwa kama ni mafunzo endelevu (CPD hours)”, alibainisha Mhe. Nchemba.
Aliongeza kuwa Mheshimiwa Mbunge ambaye ni Mwanachama wa NBAA ataingia kwenye akaunti yake, atapandisha ratiba ya kikao husika na uthibitisho wa mahudhurio katika mkutano husika ili masaa yake yahesabiwe.
Mhe. Dkt. Nchemba alifafanua kuwa ni jukumu la mwanachama mwenyewe kuingia kwenye mfumo, na siyo mtu mwingine (third party) na kutoa uthibitisho huo kwenye mfumo wa NBAA.
Post A Comment: