Na Fredy Mgunda, Lindi.
Chama kikuu cha ushirika cha RUNALI kimeanza ujenzi wa hoteli ya kisasa katika wilaya ya Liwale, lengo likiwa ni kuongeza mapato ya chama hicho kupitia vitega uchumi vipya.
Ujenzi huu utasaidia si tu kuongeza kipato cha chama, bali pia kuimarisha uchumi wa maeneo ya jirani.
Akizungumza wakati wa ziara ya viongozi wa AMCOS kutoka mkoa wa Pwani, Mwenyekiti wa RUNALI, Odas Mpunga, alielezea kuwa hatua hii ni sehemu ya mkakati wao wa kujenga na kuendeleza miradi itakayowafaidi wanachama na kuimarisha sekta ya ushirika katika wilaya ya Liwale na maeneo mengine.
Aliongeza kuwa ni muhimu kwa chama hicho kuendelea kuwa na miradi itakayowasaidia kuongeza mapato na kuboresha huduma kwa wanachama.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika cha Pwani (CORECU), Mussa Hemedi mng'eresa, alielezea furaha yake kwa kuona mafanikio ya RUNALI na kusema kuwa wao pia wanajivunia mafanikio haya. Alisema kuwa wamepanga kuanzisha miradi ya maendeleo katika chama chao, wakifuata mfano mzuri unaoonyeshwa na RUNALI, na kuwa hiyo ni ishara ya maendeleo endelevu katika sekta ya ushirika.
Miradi hii ya maendeleo inaonyesha juhudi za vyama vya ushirika katika kuboresha hali ya maisha ya wanachama na kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa mikoa mbalimbali, hasa kupitia uwekezaji katika sekta za kitalii na huduma za kijamii.
Post A Comment: