Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa Paul Christian Makonda, ameongoza wananchi na viongozi mbalimbali wa mkoa huo katika kampeni maalum ya usafi wa mazingira na upandaji miti, iliyofanyika leo katika Kata ya Ambureni, Halmashauri ya Meru. Tukio hilo limefanyika kama sehemu ya maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa, likilenga kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kuhifadhi uoto wa asili.
Katika hotuba yake, Mhe. Makonda ametoa maagizo madhubuti kuhusu utunzaji wa miti na mazingira, akisisitiza kuwa mtu yeyote anayehitaji kukata mti atapaswa kupata kibali kutoka ofisi za halmashauri husika
"Kuanzia sasa, hakuna mtu atakayekata mti kiholela. Yeyote anayehitaji kufanya hivyo lazima apate kibali kutoka ofisi za halmashauri. Hatutaki kuona miti inakatwa bila mpangilio na kusababisha uharibifu wa mazingira."
Aidha, ameongeza kuwa mtu yeyote anayefanya maombi ya kibali cha ujenzi ni lazima aonyeshe sehemu atakayopanda miti kama sehemu ya wajibu wake wa kuhifadhi mazingira.
"Hakuna kibali cha ujenzi kitakachotolewa bila mwombaji kuonyesha ni wapi atapanda miti. Tunataka kuhakikisha kuwa maendeleo ya miji na vijiji vyetu yanaenda sambamba na uhifadhi wa mazingira."
Wananchi na viongozi waliohudhuria kampeni hiyo walishiriki zoezi la upandaji miti na kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya Kata ya Ambureni, wakionesha mshikamano wa pamoja katika kuhakikisha mazingira yanabaki safi na salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Post A Comment: