Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumanne Februari 25, 2025 , amezindua rasmi Jengo la Halmashauri ya Mji wa Handeni huku akisisitiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma kote nchini.

Rais Samia amewataka watumishi wa halmashauri kuzingatia majukumu yao na kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi bila kujiona kuwa juu yao. 

"Yale makoti mtakayovaa na mabrificase mtakayobeba yasiwapandishe mabega. Nyinyi ni watumishi wa wananchi hawa," alisisitiza.

Jengo hilo ni mojawapo ya majengo 122 yaliyojengwa ndani ya miaka minne, ikiwa ni juhudi za serikali kuhakikisha huduma zote zinapatikana ndani ya kituo kimoja, kuondoa usumbufu kwa wananchi. 

"Tunafanya hivi ili watumishi wawe na sehemu bora za kufanyia kazi na wananchi wapate huduma kwa urahisi," alisema Rais Samia.

Rais Samia pia amesisitiza umuhimu wa ulipaji kodi ili kufanikisha maendeleo ya nchi. 

"Miradi yote tunayotekeleza, iwe ni barabara, vituo vya afya, hospitali, au miradi mingine inatokana na kodi zenu. Tunalinda haki ya kila mwananchi kulipa kodi stahiki bila kubambikiziwa, lakini pia msidhulumu kodi za serikali," alisema.

Ameongeza kwa kusema, kuwa serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato na kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha.

 “Kodi ni kwa manufaa yetu, tozo ni kwa manufaa yetu. Tunapokusanya kodi kwa uadilifu, tunaweza kuleta maendeleo makubwa zaidi kwa wananchi,” alisisitiza.

Vilevile, Rais Samia ameeleza kuwa, serikali inatekeleza miradi ya barabara za lami na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme Handeni, kitakachoongeza upatikanaji wa umeme kwa wananchi na miradi ya maendeleo.

Rais Samia pia amewakumbusha wananchi kujiandikisha kwenye daftari la wapigakura ili kushiriki uchaguzi wa Oktoba mwaka huu.

Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, amesema serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 391 kwa halmashauri 122 nchini kwa ajili ya ujenzi wa majengo kama hayo ambapo katika Mkoa wa Tanga pekee, serikali imetenga zaidi ya bilioni 24 kwa ujenzi wa miundombinu muhimu, ikiwemo soko na stendi mpya katika Kata ya Chanika, Handeni.










Share To:

Post A Comment: