Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa Mkoa wa Tanga unakwenda kuwa kitovu cha uchumi wa kimataifa kwa uwekezaji mkubwa unaofanyika, ukiwemo ujenzi wa barabara kuu, uboreshaji wa bandari, viwanda vikubwa na miundombinu ya kisasa inayounganisha Tanzania na nchi jirani.

Akizungumza leo Jumatano, Februari 26, 2025, katika mkutano wa hadhara wilayani Pangani mkoani Tanga, Rais Samia ameeleza dhamira yake ya kuifungua Tanga kiuchumi kupitia miradi mikubwa ya maendeleo, huku akisisitiza kuwa barabara ya Bagamoyo - Makurunge - Mkange - Pangani - Tanga itakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Pangani na ukanda wa Pwani.

“Nimeweka jiwe la msingi la barabara hii kwa sababu tunataka uchumi wa Pangani ubadilike. Lakini zaidi, tunataka kuiunganisha Tanga na mikoa mingine, kanda za kiuchumi na shoroba kuu za biashara. Barabara hii inaunganisha Tanzania na Kenya kupitia mpaka wa Horohoro, na pia inatuunganisha moja kwa moja na Dar es Salaam, Lindi, na Mtwara,” alisema Rais Samia.

Amebainisha kuwa kupitia barabara hiyo, usafiri wa utalii na biashara utaimarika, huku ikirahisisha shughuli za wakulima wa mkonge, mihogo na nazi wa Pangani kupeleka mazao yao sokoni kwa urahisi zaidi.

Rais Samia amefafanua kuwa serikali yake inatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, ambayo itakuwa moja ya bandari kubwa zaidi Tanzania, sambamba na eneo huru la kiuchumi na kongani ya viwanda.

"Bagamoyo tunakwenda kujenga eneo huru la kiuchumi na bandari kubwa ya kisasa. Tunaiunganisha Tanga na Bagamoyo ili kuwe na mtiririko mzuri wa biashara na uwekezaji, na hatimaye tutafungua fursa zaidi za kiuchumi kwa wananchi," alieleza.

Kwa upande wa sekta ya kilimo na viwanda, Rais Samia ametangaza mpango wa kujenga kiwanda kikubwa cha sukari ndani ya Mkoa wa Tanga, huku mashamba makubwa ya miwa yakipandwa katika bonde la Pangani.

"Viwanda vingi vya sukari vinazalisha sukari tunayokula, lakini tunataka pia kuzalisha sukari ya viwandani ambayo kwa sasa tunaagiza kutoka nje. Tumeamua kiwanda hiki kijengwe ndani ya Tanga karibu na bandari, na mashamba makubwa ya miwa yatakuwa Pangani. Hii ni fursa ya ajira kwa vijana wa Tanga," alisema Rais Samia.

Ameongeza kwa kusema kuwa, serikali pia inajenga soko la kimataifa la samaki Kipumbwi, hatua itakayochochea uchumi wa buluu na kuongeza mapato kwa wavuvi wa Pangani na Tanga kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amegusia mpango wa kuboresha usafiri wa majini ili kuiunganisha Tanga, Unguja na Pemba.

"Tayari sekta binafsi imeanza safari kati ya Unguja, Tanga na Pemba kupitia boti za ZanFerries. Naagiza safari hizi ziongezwe pamoja na idadi ya boti ili kuimarisha biashara na usafiri kati ya pande hizi," alisema.

Aidha, amekabidhi boti 35 za uvuvi kwa wavuvi wa Tanga, ambapo kila boti moja ina uwezo wa kubeba tani 3 hadi 5 za samaki, hatua itakayoongeza mavuno ya baharini na kuboresha kipato cha wavuvi.

Rais Samia ameiagiza Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha kilometa 8 za barabara kuu zinazoelekea Pangani zinakamilika haraka.

"Wananchi wa Pangani wamenieleza mahitaji yao, na fedha zipo tayari. Naomba Waziri wa Ujenzi ahakikishe mkandarasi anamaliza kazi haraka," alisisitiza.

Mwisho, amehimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura, akisema ni muhimu kwa kila Mtanzania kuwa na haki ya kushiriki kikamilifu katika maamuzi ya nchi.

Kwa miradi hii mikubwa ya barabara, bandari, viwanda na soko la kimataifa, Mkoa wa Tanga unazidi kuimarika kama kitovu cha uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki, huku serikali ya Rais Samia ikiendelea kusukuma mbele maendeleo kwa kasi isiyo na kifani.

















Share To:

Post A Comment: