RAIS Dkt Samia Suluhu Hassan,amerudisha matumaini kwa wananchi wa kijiji cha Kimbanga Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma,baada ya kutoa kiasi cha Sh.milioni 60 kwa ajili ya kuchimba kisima cha maji ili kumaliza kero ya huduma ya maji safi na salama iliyokuwepo kwa muda mrefu katika kijiji hicho.
Kwa sasa,wakazi wa kijiji cha Kimbanga wanatembea umbali wa kilometa 1 hadi 2 kila siku kwenda vijiji vya jirani kutafuta maji,jambo linalowarudisha nyuma kimaendeleo licha ya kuwa wakulima wazuri wa mazao ya chakula na biashara ikiwemo zao maarufu la Kahawa.
Akizungumza na wakazi wa kijiji hicho Kaimu Meneja wa Ruwasa Wilayani Nyasa Athuman Chola alisema,Ruwasa Wilaya ya Nyasa imepokea Sh.milioni 300 zilizoletwa na Rais Samia Suluhu Hassan ili kuchimba visima vya maji katika vijiji vitano ikiwemo kijiji cha Kimbanga.
Alisema,katika kijiji cha Kimbanga kazi ya kuchimba kisima imekamilika na sasa wanaendelea kujenga kioski cha kuchotea maji ambacho ujenzi wake umefikia asilimia zaidi ya 40.
Chalo ametaja kazi ya zilizobaki ni kusambaza mabomba ya maji kwenda kwenye makazi ya Wananchi,kujenga vituo vya kuchotea,kufunga mashine ya kusukuma maji kutoka kwenye kisima na kupeleka kwenye tenki na kufunga umeme jua.
“mpaka sasa tumefanikiwa kuchimba kisima katika Kijiji cha Kimbanga pekee na kwenye vijiji vinne tumeshindwa kupata maji chini ya ardhi,hata hivyo tutatumia njia mbadala ikiwemo kuboresha chamchem na kujenga miradi ya mserereko kwa kutoa maji milimani na kupeleka kwa wananchi”alisema Chola.
Aidha alisema,katika kijiji cha Malamala wanaendelea kufanya usanifu upya kwani imeshindikana kupata chanzo cha maji cha uhakika na watashirikiana na mamlaka ya Bonde la Ziwa Nyasa ili wananchi waweze kupata maji ya uhakika.
Ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,kwa kutenga fedha ili kutekeleza miradi ya maji katika vijiji mbalimbali ambayo inalenga kupunguza na kumaliza kabisa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.
Baadhi ya Wakazi wa kijiji cha Kimbanga,wameishukuru Serikali kupitia Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kwa uamuzi wa kutatua changamoto ya maji safi na salama katika kijiji chao.
Adelius Mwingira alisema,mradi wa kisima utasaidia kuwaondolea kero ya muda mrefu ya kutumia maji ya visima vya asili ambavyo maji yake siyo safi na salama pamoja na mateso ya kubeba ndoo za maji kichwani kila siku.
Bonus Kapinga alisema,mradi wa kisima ni ukombozi mkubwa kwao kwa sababu kijiji hicho tangu kilipoanzishwa miaka zaidi ya 50 hakijawahi kupata mradi wa maji ya bomba badala yake wanatumia maji kutoka vyanzo vingine vya asili kama mito na mabonde yanayop kando kando ya kijiji hicho.
Alisema,kero hiyo inasababisha hata maendeleo ya kitaalum kwa wanafunzi wa shule ya msingi kuwa chini kwa kuwa muda wa masomo wanafunzi wanakutumia kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
William Komba,ameishukuru Serikali kupeleka mradi wa kisima cha maji,lakini ameiomba Serikali kupitia Ruwasa kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa kisima hiko haraka na kufikisha mtandao wa maji kwenye makazi ya wananchi ili wasiendele kuteseka kwa kutembea umbali mrefu hadi kwenye vituo vya kuchotea maji.
Mafundi wakiendelea na ujenzi wa kioski cha kuchotea maji katika kijiji cha Kimbanga Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma kupitia mradi wa uchimbaji visima 900/5 kwa kila Jimbo ambapo Wilaya ya Nyasa imepata visima vitano vitakavyochimbwa kwa gharama ya Sh.milioni 300.
Post A Comment: