Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Jumatano Februari 26, 2025 amekabidhi boti 35 za kisasa kwa wavuvi wa Mkoa wa Tanga, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi wa ukopeshaji wa boti kwa wavuvi nchini.
Mradi huu, unaosimamiwa na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, unalenga kusaidia wavuvi katika Ukanda wa Pwani, Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa ili kuongeza tija katika sekta ya uvuvi na kuhakikisha uvuvi endelevu.
Awamu ya kwanza ya mradi huu ilianza mwaka wa fedha 2022/2023 kwa gharama ya shilingi bilioni 11.5, ambapo boti 160 zilikopeshwa kwa wanufaika 3,163.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Ashatu Kijaji, amesema kuwa boti hizo zitasaidia si tu kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi, bali pia kudhibiti uvuvi haramu. Alieleza kuwa vijana 113 kutoka Mkoa wa Tanga, ambao hapo awali walijihusisha na uvuvi haramu, wameamua kubadili maisha yao na sasa wanajiunga na vikundi vya uvuvi halali kupitia mpango huu wa mikopo nafuu.
Katika bajeti ya mwaka 2024/2025, Serikali imetenga boti 120 kwa ajili ya wavuvi, ambapo boti 70 zitapelekwa Ukanda wa Pwani (Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi, na Mtwara), boti 29 zitapelekwa Ziwa Victoria, na boti 21 zitapelekwa Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa.
Boti 35 zilizokabidhiwa leo zina thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 4.477, na moja ya boti hizo imekabidhiwa kwa kikundi cha vijana wa Tanga, ambao wameahidi kuwa walinzi wa rasilimali za uvuvi ndani ya taifa.
Huu ni mwendelezo wa juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuinua sekta ya uvuvi na kuhakikisha kuwa wavuvi wanapata nyenzo bora za kazi kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Post A Comment: