Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema lengo la kujenga barabara unganishi ya Tanga- Pangani-Bagamoyo pamoja na Daraja la Pangani aliloliwekea jiwe la msingi mapema leo Februari 26, 2025 ni kutaka kuifungua Tanga kiuchumi na kiutalii ili kuhakikisha wananchi wa Tanga wananufaika na rasilimali na fursa mbalimbali zilizopo Mkoani humo.
Rais Samia Suluhu Hassan anayeendelea na ziara yake ya Kikazi mkoani Tanga amebainisha hayo mapema leo Wilayani Pangani Mkoani Tanga wakati akizungumza na wananchi wa Pangani, akisisitiza umuhimu wa wananchi wa Tanga kufaya kazi kwa bidii ili kuhakikisha wanakuwa wanufaika wakubwa wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa Mkoani humo.
Rais Samia ameeleza kuwa Ujenzi wa barabara ya Kiwango cha Lami itakayounganisha Pangani- Tanga na Bagamoyo, kutaiunganisha Tanga na kanda kadhaa za kiuchumi ikiwemo Kanda ya Bagamoyo, sehemu ambayo kunajengwa eneo huru la kiuchumi (Kongano la viwanda) ambayo itakuwa kubwa zaidi kuliko zote zilizowahi kujengwa nchini Tanzania, sambamba na ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo.
Rais Samia pia ameeleza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutawanufaisha wakulima wa Pangani Mkoani Tanga ambao wengi wao wanajishughulisha na kilimo cha Mihogo, Mkonge na nazi kwani barabara hiyo itakuza masoko ya bidhaa zao za kilimo pamoja na kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara mbalimbali.
Post A Comment: