NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

KUPITISHWA kuwa Sheria kuhusu nyongeza ya siku za likizo kwa Wafanyakazi wanawake wanaojifungua watoto njiti inaenda kusaidia kulinda ustawi wa watumishi wanaojifungua Watoto njiti nchini kwani jambo hilo lilikuwa ni changamoto kubwa na kilio cha muda mrefu cha Wafanyakazi Wanawake.

Mtandao wa Haki ya Afya ya Uzazi nchini (SRH) unaoongozwa na Doris Mollel Foundation kwa pamoja na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) wametoa pongezi kwa Serikali kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia na kupitisha kuwa sheria jambo hilo.

Ajizungumza na waandishi wa habari leo Februari 3, 2025 Jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti TUGHE, Dkt. Jane Madete amesema hatua hiyo itasaidia kulinda ustawi wa watumishi wanaojifungua Watoto njiti nchini kwani jambo hilo lilikua ni changamoto kubwa na kilio cha muda mrefu cha Wafanyakazi Wanawake wanaopata changamoto ya kujifungua watoto njiti.

Amesema wafanyakazi wanawake wanaojifungua watoto njiti wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali ikiwemo za kiafya hivyo wanahitaji kupata muda mwingi wa kupumzika na pia kumuhudumia mtoto toka katika kipindi cha uangalizi hadi wanaporuhusiwa kutoka hospitalini.

"Mbali na changamoto ya kiafya pia wamekuwa kwenye wasiwasi mkubwa wa kupoteza Ajira zao jambo ambalo linaweza kupelekea msongo wa mawazo na hata kuathiri kwa kiasi kikubwa malezi ya mtoto aliyezaliwa". Amesema

Aidha amesema kuwa kufuatia nyongeza ya siku za likizo itasaidia wanawake hao wanaokutana na changamoto hiyo kupata muda wa kutosha kuhudumia mtoto/watoto na pia kuimarisha afya yake katika kipindi chote cha likizo pasipo kuwa na wasiwasi wa kupoteza ajira yake.

Amesema kuwa pia mama huyo atakaporejea kazini afya yake itakuwa imara zaidi na kufanya kazi kwa ufasaha na kuleta tija katika eneo lake la kazi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel, Doris Mollel amesema ni jambo jema kuona serikali inaendelea kuunga mkono juhudi za kusaidia mtoto njiti na Tanzania itakuwa nchi ya kwanza Afrika kupata mabadiliko haya katika sheria hii ambayo inaweka ustawi wa watoto njiti katika mazingira salama.

Amesema hadi kufikia mafanikio haya wamekuwa wakipambana kwa muda mrefu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo TUGHE hadi kufikia hivi sasa.

“Tunawashukuru TUGHE ambao walikuwa tayari kulipokea wazo na kulifanya kuwa la kwao, kwahiyo sasa likahama kutoka wazo la taasisi moja na kuhamia kwao, hii imetufunza kuwa kufanya kazi peke yako utafanikiwa kwa kuchelewa zaidi lakini mkiwa wengi inakuwa ni rahisi". Amesema Doris.

Pamoja na hayo Doris amewapongeza Wabunge wanawake, Umoja wa Wenza wa Viongozi "Ladies of New Millenium Women Group" pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kutoa ushirikiano wa kutosha kuweza kusaidia jambo hilo.

Nae Mwakilishi kutoka Shirika la Women Fund Tanzania (WFT), Agness Mtuhi amesema suala la elimu limekuwa ni changamoto kwani katika maeneo ya vijijini wengine hawaelewi maana ya watoto njiti, baadhi ya shuhuda za kinamama wamekuwa wakikiri kuogopa watoto wanaowazaa na wakitamani kuwatupa.

Huko vijijini bado tuna kazi ya kuendelea kutoa elimu kuwa watoto njiti ni kama wengine na wanaweza kuishi na kupata elimu inayotakiwa,kuliko kukata tamaa na kudiriki kutaka kuwatupa pindi wanapojifungua”. Amesema 
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: