Njombe imeendelea kufanya vizuri katika sekta ya elimu kwa mwaka 2024/2025, ikiwa miongoni mwa mikoa iliyopata mafanikio makubwa katika matokeo ya mitihani ya upimaji wa Darasa la Nne na ule wa kumaliza Darasa la Saba. Haya yamebainishwa katika kikao cha tathmini ya matokeo hayo, ambacho kimewakutanisha walimu wakuu wa shule za msingi na maafisa elimu wa mkoa, kwa lengo la kujadili mbinu za kuimarisha ufaulu zaidi kwa mwaka 2025/2026.

Akizungumza katika hafla ya utoaji wa vitabu vya ziada kwa shule za msingi na sekondari, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amepongeza juhudi za walimu na maafisa elimu katika kuinua viwango vya ufaulu mkoani humo. Amesema mafanikio haya ni ishara ya mshikamano baina ya serikali, walimu, wazazi na wadau wa elimu.

“Hatuwezi kuficha mafanikio haya—Njombe inazidi kung’ara katika sekta ya elimu. Tunashuhudia ongezeko la ufaulu kwa kasi nzuri, jambo linaloonyesha kuwa juhudi zetu za kuwekeza katika elimu zina matokeo chanya. Nawapongeza walimu na maafisa elimu kwa kazi kubwa wanayoifanya,” alisema Mhe. Mtaka.

Katika hafla hiyo, Mhe. Mtaka pia alipokea vitabu vya ziada vilivyotolewa na mdau wa elimu, Africa Proper Education Network, kama zawadi kwa jitihada zake za kuimarisha sekta ya elimu mkoani Njombe. Alimpongeza mdau huyo kwa kuona umuhimu wa kushirikiana na serikali katika kuinua ubora wa elimu.

“Elimu ni msingi wa maendeleo yetu, na tunapopata wadau wanaojitoa kwa dhati kama Africa Proper Education Network, ni faraja kubwa. Hii ni ishara kwamba elimu si jukumu la serikali peke yake, bali ni wajibu wa jamii nzima,” aliongeza Mkuu wa Mkoa.

Aidha, Mhe. Mtaka ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada kubwa za kuboresha miundombinu ya elimu nchini, ikiwemo ujenzi wa shule mpya, madarasa, mabweni na uwezeshaji wa walimu.

“Serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeongeza na kuboresha kwa kiwango kikubwa miundombinu ya elimu, hali inayowapa wanafunzi mazingira bora ya kujifunzia na walimu mazingira mazuri ya kufundishia. Haya ni mafanikio makubwa tunayopaswa kuyathamini na kuyatumia kikamilifu ili kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bora,” alisisitiza Mhe. Mtaka.

Katika kikao hicho, walimu na maafisa elimu walikubaliana kuongeza juhudi zaidi ili kuhakikisha ufaulu wa wanafunzi unaendelea kuimarika kwa mwaka 2025/2026, huku ushirikiano wa wadau wa elimu ukiendelea kupewa kipaumbele.







Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Post A Comment: