Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo amefichua taarifa za wizi wa fedha kiasi cha sh252milioni zilizobambikwa kwenye mahitaji ya manunuzi ya eneo la ekari sita kwa ajili ya ujenzi wa shule katika kata ya Muriet jijini Arusha.
Wizi huo unadaiwa kutaka kutekelezwa na baadhi ya watendaji wa halmashauri ya jiji la Arusha, baada ya kudai kiasi cha Sh552milioni kwa ya ununuzi wa eneo hilo badala ya thamani halisi ambayo ni sh300milioni.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa wananchi wa mtaa wa Muriet Mashariki kwenye eneo hilo lililonunuliwa, Gambo amesema kuwa eneo hilo lilikuwa linunuliwe kwa mda mrefu lakini kutokana na mvutano wa kuokoa fedha za serikali ilisababisha lichelewe.
Aidha eneo hilo lililokuwa linunuliwe mwaka 2022 limefanikiwa kununuliwa desemba mwaka jana 2024 .
“Tunatambua changamoto mnayopitia lakini kuna changamoto hizo za fedha kutaka kupigwa ndio maana tukasimama kidete kutetea wizi wa zaidi ya sh 252 ambazo zilitaka kupigwa na baadhi ya watendaji ambao sio waaminifu baada ya kusema eneo linauzwa sh552 milioni badala ya thamani halisi ya sh300milioni” amesema Gambo.
“Tumefanya hivyo kwa sababu tunathamini namna ambavyo Rais wetu (Samia Suluhu Hassan) anavyohangaika dunia nzima kutafuta fedha kwa ajili ya kuwahudumia watanzania, hivyo ni wajibu wetu kama wasaidizi wake kuzisimamia, kuzilinda ili zikatumike kwa mujibu wa malengo” amesema Gambo.
Amesema kuwa eneo hilo sasa limelipiwa rasmi kuwa ni eneo la serikali kwa ajili ya kujengewa wananchi shule
"Kama Kuna mtu anabisha eneo hili sio mali ya serikali tuliosimamia kidete aje aseme hapa, sio wanakuja wanapiga mboyoyo tu hapa, maneno maneno meengi halafu vitendo hamna...wao kazi yao kupiga hadithi halafu kazi ya kujenga shule wanatuachia sisi" amesema Gambo.
Nae mwenyekiti wa Maendeleo ya huduma za jamii jiji la Arusha Issaya Doita akielezea jinsi fedha hizo zilivyotaka kuibwa amesema mwaka 2022 walipokea kilio cha uhitaji wa shule katika eneo la Muriet mashariki na baraza la madiwani kupitisha ajenda hiyo na baadae wataalamu wa manunuzi kuleta tathimini ya gharama za eneo kuwa ni sh552milioni.
“Wengi tulishtuka kutokana na asili ya eneo kuwa pembezoni, hivyo baadhi yetu akiwemo M’bunge wetu makini Mrisho Gambo tulifanya utafiti wa chinichini ndio tukagundua mnyororo wa madalali walioshirikiana na baadhi ya watendaji na madiwani wa halmashauri yetu kupandisha gharama za eneo”amesema na kuongeza;
“Tulitoa taarifa kwa Takukuru na kusitisha ununuzi wa eneo hilo huku baadhi ya watu hao wakihojiwa lakini tunashangaa hadi Leo hawajachukuliwa hatua za kisheria"
"Hata hivyo tunashukuru tulishirikiana na Mkurugenzi aliyekuwepo wakati huo Juma Hamsini kumpata muhusika wa eneo la tulinunua kwa gharama ya sh300milioni” amesema.
Nae Mkuu wa wilaya ya Arusha Joseph Mkude amesema kuwa amefurahia hatua zilizochukuliwa za kuhakikisha eneo hilo linanunuliwa na kuwa mali ya serikali kwa ajili ya kusogeza huduma ya shule karibu.
“Eneo sasa mnalo kilichobaki ni kukimbizana kuhakikisha shule mnapata ili kutatua changamoto zinazowakabilia wananchi ikiwemo watoto kutembea umbali mrefu na kuhatarisha maisha yao dhidi ya ajali za barabarani” amesema.
Akizungumza katika kikao hicho, mmoja wa wananchi wa mtaa huo Rukia Mohames ameshukuru kwa mafanikio ya ununuzi wa eneo hilo na kuwataka viongozi hao kusema lini hasa ujenzi wa shule hiyo itaanza.
“Tunashukuru kwa mafanikio hayo lakini bado watoto wetu wanateseka kwenda umbali mrefu kwenda shule kwa zaidi ya kilomita 20 huku wakikabiliana na changamoto za ajali mbalimbali na zaidi tunakuwa na gharama kubwa za kuwalipia nauli kwa zaidi ya daladala mbili hadi tatu inategemea na nafasi aliyopata” amesema Rukia.
Nae diwani wa kata hiyo Francis Mbise amesema kuwa wameshapendekeza fedha zilizobaki kiasi cha sh252 zianze ujenzi wa shule hiyo huku wakisubiri bajeti zingine zaidi.
“Uzuri jumatatu tunaingia kikao cha mapendekezo ya bajeti ya 2025/2026 hivyo tunaamini tutapitisha bajeti na kuanza utekelezaji wa ujenzi haraka” amesema.
Post A Comment: