Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), kimesaini mkataba na kampuni ya kandarasi ya Arm-Strong International Ltd ya jijini Mwanza kuanza ujenzi wa maabara tatu za sayansi katika kipindi cha miezi nane ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) katika chuo hiki.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba huo iliyofanyika Februari 20, 2024, makao makuu ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo na mgeni rasmi katika hafla hiyo, Prof. Joseph Kuzilwa, amesema hii ni hatua kubwa kwani chuo hiki kinaungana moja kwa moja na serikali katika kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya elimu.
“Nchi zenye wanasayansi wengi waliojikita katika maeneo ya utafiti na maendeleo ndiyo nchi zilizopiga hatua kubwa katika maendeleo, kwa kutambua hilo nchi yetu inaelekea huko kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali hii kupitia mradi huu wa HEET ambao sehemu mojawapo ya utekelezaji wake katika chuo hiki ni ujenzi wa maabara za sayansi. Naamini katika utekelezaji wa zoezi hili tutashirikiana pande zote ili fedha za mradi huu zitumike vizuri na kwa wakati,” amesisitiza Prof. Kuzilwa.
Aidha, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda, amesema mkataba huu unasainiwa hadharani ikiwa ni kusisitiza weledi na uaminifu katika utekelezaji wa mkataba huo ili kufanya matokeo ya mradi huo kuwa na maana kubwa na kuleta maendeleo ya moja kwa moja katika jamii zetu.
“Haya ni matokeo makubwa ya uwekezaji wa serikali yetu, uwepo wa mradi huu wa ujenzi ni sehemu ya maeneo saba ya utekelezaji wa mradi wa HEET. Tunajenga maabara za sayansi sababu tunatambua nchi haiwezi kuendelea au kubadilika bila kuweka msisitizo kwenye sayansi,” amesema Prof. Bisanda.
Naibu Makamu Mkuu wa OUT katika Taaluma, Utafiti na Huduma za Ushauri wa Kataalamu. Prof. Alex Makulilo, amesema utekelezaji wa Mradi wa HEET katika chuo hiki umegawanyika katika vipengele mbalimbali, ambapo asilimia 75 ya mradi mzima zinaenda kwenye ujenzi wa maabara saba katika Kanda saba za nchi ambazo ni Arusha (Kaskazini), Mwanza (Kanda ya Ziwa), Kigoma (Magharibi), Morogoro (Kati), Njombe (Nyanda za Juu Kusini), Mtwara (Kusini) na Pwani (Ukanda wa Pwani).
Ameendelea kusema katika mkataba huu wa awali, Kampuni ya Arm-Strong International Ltd itajenga maabara tatu katika mikoa ya Arusha, Mwanza na Kigoma. Maabara nyingine zinazosalia zitajengwa na wakandarasi tofauti tofauti ambao mikataba yao itaingiwa hivi karibuni.
Mwanasheria wa Chuo, Wakili Nelly Moshi, ameomba pande zote kuhakikisha zinatekeleza na kufuata sheria zilizowekwa katika mkataba huo ikiwamo umalizaji wa kazi husika ndani ya muda ili kuondoa mivutano isiyo na lazima wakati wa utekeleaji wake.
Naye Ndg. Pastory Masota, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Arm-Strong International Ltd, amesema wao kama watekelezaji wa mradi huo watahakikisha mradi unatekelezwa vyema kama waliyokubaliana katika mkataba na wanatarajia kupata ushirikiano kutoka katika pande zote za wahusika wa utekelezaji wa mradi huo ili fedha za mradi huu zitumike vyema na kwa wakati.
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, ni miongoni mwa vyuo vikuu nchini vinavyotekeleza mradi wa HEET chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia, ambapo chuo hiki kimepata tengeo la thamani ya dola milioni tisa ambalo sehemu mojawapo ya utekelezaji wake ni ujenzi wa maabara za sayansi ambazo mkataba wake umesainiwa na tayari kwa kuanza ujenzi.
Post A Comment: