Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Mhe. Mrisho Gambo, Leo Jumatano Februari 19, 2025 wakati akizungumza na na Wazee wa Wilaya ya Arusha amehimiza wananchi wa Mkoa wa Arusha kumchagua kwa kishindo Rais Samia Suluhu Hassan kwenye uchaguzi Mkuu ujao, akisema Mkutano Mkuu wa CCM haukukosea kumpitisha kuwa Mgombea pekee kwenye uchaguzi huo.

Mhe. Gambo ambaye amekutana na Wazee hao kama sehemu ya utaratibu wake wa kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii katika kuwapatia elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ambapo pia amegawa majiko ya gesi kwa wazee 182 waliohudhuria Mkutano huo, amesema ndani ya Miaka minne ya utawala wa Rais Samia Mkoa wa Arusha na hususan Jimbo la Arusha mjini wamekuwa wanufaika wakubwa wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Akiitaja baadhi ya miradi hiyo, Gambo amesema kata ya Sombetini, Osunyai na Ungalimited ni miongoni mwa wanufaika wa miradi mikubwa ya barabara ikiwemo barabara ya Mbauda- Simanjiro, ambayo itajengwa kwa kiwango cha Lami kwa njia nne, suala ambalo litaondoa changamoto ya usafiri na usafirishaji hasa nyakati za mvua.

Ameizungumzia pia barabara ya Kilombero mpaka uwanja wa ndege wa Arusha (Kisongo) ambayo ujenzi wake ulikuwa ukisuasua tangu mwaka 2020, na Rais Samia alipoingia madarakani tayari usanifu umefanyika, fidia ya Bilioni 10 imeshaanza kulipwa kwa wananchi na tayari mchakato wa ujenzi wake umeanza katika jitihada za kuondoa msongamano wa magari kwenye Jiji hilo la Arusha sambamba na kuondoa usumbufu kwa wanaofika Jijini Arusha kwa kutumia uwanja wa ndege wa Arusha wakiwemo watalii.

Mhe. Gambo ameeleza pia kuwa Rais Samia ndani ya miaka minne ya Uongozi wake amefanikisha kuupeleka mradi wa TACTICS jijini humo, mradi ambao utajenga Kituo kikubwa cha kisasa cha mabasi Jijini Arusha, soko la Kilombero pamoja na ujenzi wa soko la Morombo ambapo kufikia mwezi wa sita mwaka huu, mkandarasi atakuwa amepatikana na kuanza kazi mara moja.

Share To:

Post A Comment: