Serikali kupitia Wizara ya Fedha imewashauri wazazi na walezi kuwafundisha Watoto kuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba ili kuwasaidia katika Maisha yao ya baadae.
Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bi. Dionensia Mjema, wakati wa semina zinazoendelea katika miji na vijiji mkoani Kilimanjaro, ikiwemo Shule za Sekondari, Mangi Mariale iliyopo Kata ya Mwika Kusini na Mwika Sekondari iliyopo Kata ya Mwika Kaskazini Wilaya ya Moshi Vijijini.
Bi. Mjema alisema kuwa kuwafundisha Watoto kuweka akiba kutawajengea mfumo madhubuti wa kujenga uhakika wa masuala ya kifedha.
“Watoto wengi wamekiri kwamba walikuwa hawafahamu kwamba wanapopewa pesa wanatakiwa watumie kiasi na kiasi kingine waweke kama akiba ili siku wazazi wao wanapokosa pesa za kuwapa waweze kuzitumia.” Alisema Bi. Mjema.
Bi. Mjema alisema kuwa kwa sasa kuna Taasisi mbalimbali kama vile Benki, Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja inayoendeshwa na UTT AMIS zinatoa elimu kwa Watoto kuhusu namna ya kuweka akiba, hivyo ni muhimu kwa wazazi na walezi kutumia fursa hizo kwa ajili ya Watoto wao.
Awali, akifundisha wanafunzi katika Shule ya Sekondari Mwika, Bi. Mjema aliwataka wanafunzi hao wawe na tabia ama utamaduni wa kupanga bajeti ili wapate akiba ya kuweka, kutoka katika fedha wanazopewa na wazazi kwa ajili ya matumizi yao ya kawaida na kununua vitu ili waweke akiba kiasi fulani cha fedha kinachobaki.
Vilevile Bi. Mjema alisema kuwa kuweka akiba ni njia za kuondokana na madeni yanayotokana na matumizi ya kila siku pamoja na gharama nyingine za maisha.
Post A Comment: