Na Mwandishi Wetu, Mbeya
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa waandaaji wa vipindi vya elimu kwa umma, kulenga zaidi kukuza uelewa na kuhamasisha jamii kushiriki shughuli za uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwa kuwakumbusha suala hilo ni wajibu wa kila mmoja.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akifunga Mkutano wa 109 wa Mwaka wa Watayarishaji wa Vipindi vya Elimu kwa Umma uliyofanyika katika Ukumbi wa City Park mkoani Mbeya. Amesema jukumu la kuhamasisha utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi ya kupikia ni kubwa na linahitaji nguvu ya pamoja inayojumuisha vyombo vya habari na wadau wote.
Amesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kuifanya agenda ya usafi na utunzaji wa mazingira pamoja na matumizi ya nishati safi kuwa sehemu muhimu ya programu zao badala ya kusubiri matukio, kama milipuko ya magonjwa, moto kwenye hifadhi za misitu au mafuriko.
Makamu wa Rais amewahimiza watayarishaji wa vipindi vya elimu kwa umma, kujizatiti kujifunza zaidi na kutoa elimu kwa usahihi kuhusu mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia yanayoendelea duniani na hivyo kuwahamasisha watanzania kuchangamkia teknolojia mbalimbali zinazoibuka, kama vile matumizi ya Akili Mnemba, roboti na matumizi salama ya mitandao.
Hali kadhalika, Makamu wa Rais amewasihi watumiaji wa mitandao kuzingatia maadili ya sekta ya habari, sheria, pamoja na mila na desturi za Tanzania zinazolinda heshima na utu. Amesema wapo baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaotoa taarifa bila kujali utu na heshima ya binadamu wengine kwa kutumia kudhalilisha na kuumiza wengine.
Pia ametoa rai kwa watayarishaji wote wa vipindi vya elimu kwa umma kuzingatia matumizi sanifu na sahihi ya lugha adhimu ya Kiswahili. Amewataka kuwa mabalozi wa Kiswahili sanifu na fasaha kwenye maeneo ya kazi na kuhakikisha wanakuwa vinara wa kupeleka Kiswahili sanifu na fasaha duniani na kuutangaza Utamaduni wa Mtanzania Kimataifa kupitia lugha na fasaha ya Kiswahili.
Makamu wa Rais amewaasa washiriki wa Mkutano huo kujiepusha na habari zitakazoibua taharuki na migogoro isiyo na tija kwa Taifa. Amewasihi kutoa taarifa zinazogusa maslahi ya wananchi ikiwemo elimu ya uraia na uchaguzi katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, Oktoba 2025 na hasa kuwakumbusha watanzania kuhusu umuhimu wa kutunza amani na utulivu katika nchi.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amesema kutokana na juhudi zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita usikivu wa redio ya Taifa umeongezeka kutoka asilimia 54 mwaka 2016 hadi asilimia 87 mwaka 2024. Ametoa wito kwa wadau wa elimu kwa umma kutumia usikivu wa redio kutangaza shughuli mbalimbali zinazofanywa na serikali ikiwemo miradi ya kimkakati na miradi ya huduma za jamii hususani maeneo ya vijijini ili kuwapa wananchi uelewa wa kutosha namna serikali inavyowahudumia.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania Dkt. Ayub Rioba amesema kauli mbiu ya mwaka huu ambayo ni “Tumia nishati safi na Tunza mazingira” inaenda sambamba na vipaumbele vinavyosimamiwa na Serikali. Amesema TBC imechukua suala la nishati safi na usafi wa mazingira kwa umuhimu mkubwa kwa kutambua suala hilo lina maslahi kwa Taifa.
Mkutano wa Wadau wa Elimu kwa Umma unaondaliwa na Shirika la Utangazaji Tanzania hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuwajengea uwezo maafisa uhusiano na mawasiliano ili waweze kuwahabarisha wananchi kwa weledi zaidi kuhusu shughuli na miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali. Mkutano huo wa 109 umehudhuriwa na washiriki zaidi ya 280 wakiwemo watendaji wakuu wa taasisi, mashirika, wakala na idara za serikali pamoja na maafisa mahusiano na mawasiliano.
Post A Comment: