Na Oscar Assenga, TANGA

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi INEC imetoa Kibali 157 kwa Asasi za Kiraia kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la kudumu kwa wapiga kura.

Hayo yalisemwa leo na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele wakati akifungua mafunzo ya uboreshaji wa daftari la kudumu kwa wapiga kura mkoa wa Tanga.
Yakiwahusisha Mratibu wa Uandikishaji Mkoa,Maafisa Uandikishaji,Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi,Maafisa Ugavi na Maafisa Tehama wa Halmashauri

Aliema pia wametoa kibali kwa taasisi na asasi za kiraia 42 kuwa waangalizi watakaoshiriki katika zoezi la uboreshaji wa daftari ambapo kati ya hizo taasisi tisa ni za kimataifa na 33 ni za ndani ya nchi.

“Nisisitize kwa maafisa waandikishaji wanapofika kwenye maeneo yenu muwape ushirikiano kwa kuwa ni wadau muhimu na vitambulisho watakavyokuwa navyo wamepatiwa na tume ni utambulisho tosha”Alisema

Aidha alisema kwamba ni muhimu wakahakikisha wanatekeleza majukumo yao kwa umakini katika eneo husika ikiwemo utunzaji wa vifaa vya uandikishaji kutokana na kununuliwa kwa gharama kubwa na vinatarajiwa kutumika kwenye maeneo mengine ya uandikishaji nchini.

“Kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa kutapelekea athari kubwa katika kukamilisha zoezi hilo muhimu lakini pia hakikisheni mnazingatia maelekezo yote yatakayotolewa na tume ili muweze kuyafanyia kazi wakati wa zoezi litakapokuwa limeanza”Alisema

Aliongeza kwamba matokeo bora ya zoezi hilo yanategemea uwepo wa ushiriki mkubwa kati ya watendaji wote wa uboreshaji, Serikali, Vyama vya Siasa na wadau wengine wa uchaguzi.

Hata hivyo alisema wakati wa uboreshaji wa daftari mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo kwenye vituo vya kuandikisha wapiga kura .

“Jambo hili ni muhimu kwani litasaidia kuleta uwazi katika zoezi zima lakini pia mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutokea vurugu zisizokuwa za lazima”Alisema

Mwenyekiti huyo wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi alisisitiza kwamba mawakala hawaruhusiwi kuwaingilia watendaji wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao vituoni.

“Maelekezo zaidi kuhusu mawakala wa vyama vya siasa yatatolewa na wakufunzi na ni muhimu kuyazingatia”Alisema

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: