Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Jumanne Gombati, amezindua rasmi
Bodi mpya ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita na kuitaka bodi
hiyo pamoja na uongozi wa hospitali kufanya kazi kwa mshikamano ili kufanikisha
malengo ya serikali ya kuboresha huduma za afya.
Akizungumza wakati wa kikao cha kwanza cha bodi hiyo, Gombati alisisitiza umuhimu wa bodi hiyo katika usimamizi wa huduma za afya na kuhakikisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
“Bodi ya ushauri ya Hospitali ya Rufani ya Mkoa, ni chombo muhimu sana
katika uendeshaji wa huduma za afya za Hospitali. Ni kiungo kinachowaunganisha
wananchi na serikali yao na kuboresha utoaji wa huduma,” amesema Gombati
“Kazi kubwa ya bodi ni kuisimamia karibu sana menejimenti ya hospitali
katika utekelezaji wa majukumu yake, kimsingi menejmenti ya hospitali
inawajibika moja kwa moja kwa bodi, hivyo wajumbe tumieni taaluma zenu
kuisaidia hospitali katika uendeshaji wa huduma za afya,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita,
Dkt. Omary Sukari, alisema bodi hiyo itasaidia kuhakikisha wananchi wanapata
wawakilishi wa kutoa maoni yao kuhusu huduma za afya zinazotolewa hospitalini
hapo.
Aidha, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa wa Geita, Dkt. Mfaume Kibwana, alieleza kuwa hospitali hiyo inaendelea
kuboresha huduma mbalimbali za kibingwa, ikiwemo huduma ya CT Scan, ambayo imepunguza rufaa za
wagonjwa kwenda hospitali za mbali.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya hospitali
hiyo, Manase Ndoroma, ameishukuru serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuwaamini
na kuwateua kusimamia hospitali hiyo. Ameahidi kuwa bodi itatekeleza majukumu
yake kwa ufanisi ili kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa Geita.
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita ilianza
kama hospitali ya halmashauri mnamo Juni 2016 baada ya Wizara ya Afya kuiteua
rasmi ili kutoa huduma za rufaa kwa mkoa pamoja na kusaidia vituo vya afya vya
ngazi za chini na taasisi za mafunzo.
Kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya mwaka 2022,
Mkoa wa Geita una wakazi 2,977,608, ambapo wanaume ni 1,463,764 na wanawake ni
1,513,844. Hospitali hii inahudumia Halmashauri za Mji wa Geita, Geita, Chato,
Bukombe, Mbogwe, na Nyang’hwale.
Post A Comment: