Shirika la Kimataifa lisilo la Kiserikali linalofanya kazi ya kuhamasisha amani,umoja na maendeleo endelevu kupitia miradi mbalimbali (Global PeaceFoundation )limezindua mradi wa jamii shirikishi katika uzalendo kwa kanda ya kusini.
Mradi huo uliopo chini ya udhamini wa ubalozi wa Netherlands umezinduliwa leo Februari 18,2025 Mkoani Lindi ambapo utatekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja ukijikita kuboresha ushirikiano baina ya vyombo vya ulinzi katika Mkoa wa Lindi hasa kwenye Wilaya ya Nachingwea na Ruvuma kwa Wilaya ya Nyasa.
Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo la Global Peace Foundation Tanzania (GPF)Hussein Sengu (Wakili)amesema malengo makubwa ya mradi huo ni kuboresha masuala ya ulinzi na usalama kwa kushirikisha polisi jamaii na wanajamii wakiwemo wanawake na vijana ili waweze kushiriki katika masuala hayo kwenye jamii zinazowazunguka.
Aidha,ameeleza kwamba kupitia mradi huo wanakwenda kuboresha mbinu na ujuzi wa kiutendaji miongoni mwa maofisa wa polisi kuhusu ulinzi shirikishi kwa kutoa mafunzo maalum kwa maofisa hao.
Balozi wa Netherlands nchini Tanzania Wiebe de Boer amesema inatia moyo kuona kila chombo kinafanya kazi na shirika hilo ili kuileta jamii karibu na kushiriki katika masuala ya ulinzi na usalama kwenye maeneo yao.
Akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi,Mkuu wa Wilaya ya Lindi Victoria Mwanziva amesema zipo dhana mbalimbali ikiwemo ya kufumbia macho matukio ya uhalifu na kuyamaliza nyumbani kimya kimya hali inayosababisha kuendelea kushamiri kwa matukio hayo na uwepo wa mradi huo wenye lengo la kuongeza ushirikiano kati ya polisi na wanajamii wanaenda kutatua hilo.
Nae,Naibu Kamisha wa Jeshi la Polisi na Mkuu wa dawati la ushirikishwaji Kamisheni ya Polisi jamii kutoka Makao Makuu ya jeshi hilo Dodoma Henry Mwaibambe,amesema wamepokea mradi huo ikiwa ni mwendelezo wa miradi walionao kwani unakwenda kufanya kazi kwenye kata ambayo tayari askari wao wapo hivyo amewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi la polisi kuibua changamoto mbalimbali kwenye jamii ambazo zimekuwa na sura ya uhalifu ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi.
Kwa upande wa wakuu wa Wilaya ya Nchingwea Mohamed Moyo na Nyasa Peres Magiri ambazo mradi huo unakwenda kutekelezwa,wameshukuru serikali ya Uholanzi wakishirikiana na Shirika la Global Peace Foundation kwa kuwapelekea mradi huo wakiamini utakwenda kuongeza uelewa na uzalendo kwa jamii na hivyo kupunguza changamoto za uhalifu katika maeneo yao hasa kwa maeneo ambayo yamekuwa yakipata mwingiliano wa watu kutoka nchi za jirani kama Msumbiji na Malawi.
Post A Comment: