Na Chedaiwe Msuya, WF, Same


Wananchi wa Kata ya Kihurio, wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kuhakikisha wanatumia huduma za Taasisi za Fedha zilizosajiliwa na kupata Leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania na zinazozingatia Sheria, Kanuni, na Taratibu zinazotumika ili kuepuka huduma za fedha kutoka kwa watoa huduma wasio sajiliwa.

Rai hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Kata ya Kihurio, Bw. Rafaeli Tomasi, alipokutana na Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha waliokwenda kutoa elimu ya fedha kwa wananchi.

Bw. Tomasi alieleza kuwa kumekuwa na baadhi ya taasisi zinazotoa mikopo kwa wananchi kwa kushindwa kufuata sheria, hali inayosababisha malalamiko ya mara kwa mara na kusababisha wananchi kupoteza mali zao walizoweka kama dhamana.

"Watoa huduma za fedha na taasisi zinazotoa mikopo hapa wilayani tumewasisitiza kwamba huduma zao zisilete madhara kwa wananchi, na tutachukua hatua za kisheria kwa yeyote atakayekiuka kanuni za kiserikali," alisisitiza Bw. Tomasi.

Akizungumzia kuhusu elimu inayotolewa na Wataalamu wa Wizara ya Fedha, Bw. Tomasi alisema kwamba elimu hiyo itawasaidia wananchi kuelewa haki na wajibu wa watoa huduma katika utoaji wa mikopo, ili waepuke mikopo inayoweza kuwaathiri vibaya.

Bw. Tomasi alisisitiza kuwa ana imani elimu hiyo itawaongezea wananchi ufahamu wa haki zao, ikiwa ni pamoja na kuelewa taratibu za mikopo, kiwango cha riba kinachotozwa na taasisi ya fedha kabla ya kuchukua mkopo.

"Tunaishukuru Wizara ya Fedha kwa kuona umuhimu wa kutoa Elimu ya Fedha mpaka ngazi ya Kata na Vijiji ili kuwafikia wananchi wengi ambao fursa hizi hawazipati na pia nampongeza Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kwa kuhakikisha  elimu hii inawanufaisha wananchi na kuwawezesha kukabiliana na changamoto za kiuchumi," aliongeza Bw. Tomasi.

Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, alisema kuwa mpango huu wa kutoa Elimu ya Fedha ni endelevu kwa kuwa sekta ya Fedha inakua kwa kasi pia kuna fursa nyingi ambazo wananchi wanatakiwa kuzifahamu na kuzitumia kwa usahihi. 

"Hatua hii inaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya kuwawezesha wanawake, vijana, walemavu, na wazee kwa elimu na kuboresha usawa wa kiuchumi nchini, ili kufanikisha maendeleo endelevu na ustawi wa Taifa na kuweza kutumia fursa za kifedha zilizopo na kuzitumia kwa usahihi," alisema Bw. Kibakaya.

Mpango wa kutoa elimu ya fedha umelenga kuwawezesha wananchi kuelewa masuala ya fedha na kuboresha ufahamu wao ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha  ya mwaka 2020/21 - 2029/30







Share To:

Post A Comment: