
Na Ashrack Miraji –
Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, ameonyesha kutoridhishwa na usimamizi wa mradi wa maji unaotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) katika Kata ya Kisiwani. Licha ya serikali kutoa shilingi milioni 720 kwa ajili ya mradi huo, bado haujanufaisha walengwa, huku baadhi ya wananchi wakidaiwa kujiunganishia maji kinyemela.
Hali hiyo ilibainika katika kikao cha wananchi wa Kijiji cha Kisiwani Barazani, ambapo msimamizi wa mradi alishindwa kutoa maelezo ya kina kuhusu gharama za mradi, idadi ya walengwa, na hatua zilizochukuliwa dhidi ya waliojiunganishia maji kinyemela. Kukosa kwake majibu kulizua maswali mengi kutoka kwa Mkuu wa Wilaya, Kamati ya Usalama ya Wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri, wataalamu, na wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Mhe. Kasilda Mgeni alieleza kutoridhishwa na hali hiyo, akisisitiza kuwa ni jambo lisilokubalika kwa msimamizi wa mradi kushindwa kueleza thamani ya fedha zilizotolewa, watu waliopaswa kunufaika, na maendeleo ya mradi.
“Yaani kimsingi umenichefua! Kama hii kazi huitaki, sema, kuna watu wanashida na hizi kazi. Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan ameleta milioni 720 hapa, na RUWASA ndio mmepewa jukumu la kuutekeleza. Thamani ya hela mliyoletewa hujui, ulilenga kunufaisha watu wangapi hujui! Hapa lazima hatua kali zichukuliwe. Haiwezekani watu wanapewa mradi mkubwa wa milioni 720, halafu mwisho wa siku maji hayatoki, wala hawajali! Hawajui wananchi wangapi wanapaswa kuhudumiwa na huo mradi, hawajui!” alisema kwa hasira.
Aidha, Mhe. Mgeni aliwataka wananchi wote waliounganisha maji kinyemela kujisalimisha mara moja kabla ya kuchukuliwa hatua kali za kisheria. Pia, aliwaagiza wenyeviti wa vijiji na watendaji wa kata kufuatilia na kuwabaini wote waliohusika katika vitendo hivyo ili wachukuliwe hatua stahiki.
“Waliojiunganishia maji, niwaombe mjisalimishe kabla hamjakamatwa. Ninyi mnafanya wenzenu wakose maji. Ninyi ni wezi kama wezi wengine wanaoiba mali za umma. Hii ni haki ya wananchi wote, si ya wachache wanaochukua kwa ujanja. Hatutavumilia hali hii, na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote waliohusika,” alisisitiza.
Mkuu wa Wilaya ameagiza RUWASA kutoa maelezo ya kina kuhusu matumizi ya fedha za mradi, idadi ya walengwa, na hatua zitakazochukuliwa ili kuhakikisha maji yanawafikia wananchi waliokusudiwa.
Mradi huo wa maji katika Kata ya Kisiwani ulilenga kunufaisha jumla ya wananchi 3,150, huku gharama halisi ya utekelezaji wake ikiwa shilingi milioni 722.2. Hata hivyo, mradi huo umeshindwa kufanikisha malengo yake kutokana na changamoto za usimamizi, jambo ambalo sasa linahitaji hatua madhubuti za ufuatiliaji na uwajibikaji.
Post A Comment: