Na. Josephine Majura, WF - Dodoma

 

Bunge limepitisha nyongeza ya mapato na matumizi ya jumla ya shilingi bilioni 945.7 kwa ajili ya kuongeza kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/25 kutoka shilingi trilioni 49.346 iliyoidhinishwa awali hadi shilingi trilioni 50.291.

 

Nyongeza hiyo imewasilishwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ambaye ameeleza kuwa fedha hizo zitakazotekeleza shughuli za sekta za elimu, afya  utalii na program mbalimbali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, zimepatikana kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

 

Alisema shilingi bilioni 325.9 zimetengewa Wizara ya Fedha, kwa ajili ya matumizi ya kitaifa, kugharamia malipo ya madeni ya watumishi, wakandarasi na wazabuni wa ndani pamoja na ujenzi wa miundombinu ya Serikali katika Mji wa Serikali Mtumba.

 

Mhe. Nchemba aliongeza kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetengewa shilingi bilioni 131.4 kwa ajili ya kugharamia mahitaji ya Mtaala mpya wa sekta ya elimu ikiwemo ujenzi wa shule za sekondari za amali, upatikanaji wa vifaa na walimu.

 

“Fedha hizo zitagharamia ukamilishaji wa ujenzi wa vyuo vya VETA, ujenzi wa maktaba ya Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), ujenzi wa miundombinu ya Chuo cha Nelson Mandela-Arusha, ujenzi wa majengo ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima pamoja na ujenzi wa Jengo la Maktaba Mwanza”, alibainisha Mhe. Dkt. Nchemba.

 

Aliongeza kuwa Wizara ya Afya imeongezewa shilingi bilioni 53.7 kwa ajili ya kugharamia dawa, vifaa tiba na vitendanishi.

 

Mhe. Dkt. Nchemba alisema Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeongezewa shilingi bilioni 173.7 kwa ajili ya sekta ya elimu, afya na kuiwezesha TARURA kukarabati miundombinu ya barabara na madaraja iliyoathirika na mvua za masika ili iweze kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

 

Alisema shilingi bilioni 260.7 zimetengwa kwa ajili ya Wizara ya Maliasili na Utalii ili kugharamia uendeshaji na ukarabati wa miundombinu ya barabara katika Hifadhi za Taasisi za Utalii za Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA.)

 

Aidha, Mhe. Dkt. Nchemba alisema mgawanyo huo umezingatia maono ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa na nguvu kazi yenye ujuzi wa kuhakikisha utekelezaji wa elimu ya amali ni unafanyika kwa vitendo.

 

Share To:

Post A Comment: