Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Kilimo na Maliasili imeipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ubunifu wake katika kuboresha sekta ya utalii kupitia miradi mbalimbali ya miundombinu.

Pongezi hizo zilitolewa leo Februari 16, 2025 wakati wa ziara ya kamati hiyo katika eneo la Mapango ya Amboni na Hifadhi ya Misitu ya Mikoko, Sahare, mkoani Tanga.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Mnzava, alisema kuwa wizara kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeonesha uwezo wa kubuni aina mpya ya bidhaa za utalii, hususan kupitia mradi wa daraja la utalii unaotekelezwa katika hifadhi hiyo.

“Mengi yameshasemwa na wajumbe wa Kamati, lakini kwa mradi huu mmetufurahisha. Nawapongeza wizara, nawapongeza TFS. Nasi tutahakikisha bajeti ya miradi kama hii inatolewa kwa wakati ili iweze kutekelezwa kwa malengo yaliyokusudiwa,” alisema Mhe. Mnzava.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, alishukuru Kamati kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za wizara katika kuboresha sekta ya utalii.

“Tunashukuru kwa namna mnavyoendelea kuipambania wizara, hususan katika vikao vya bajeti bungeni. Mafanikio haya tunayoyaona ni matokeo ya maelekezo yenu kuhakikisha miradi ya wizara na taasisi zake inatekelezwa kwa ufanisi,” alisema Dkt. Pindi Chana.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batlida Buriani, aliipongeza wizara kwa kuleta miradi ya utalii mkoani humo, akibainisha kuwa itatoa fursa zaidi za ajira na kuinua uchumi wa wakazi wa eneo hilo.

Akijibu hoja za wajumbe wa Kamati, Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo, alieleza kuwa maelekezo ya Kamati yamekuwa chachu kwa TFS kuendelea kutekeleza miradi ya kuboresha miundombinu ya utalii, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa daraja la utalii katika msitu wa mikoko kwenye pwani ya Bahari ya Hindi, Tanga.

Ziara hiyo ilihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dastan Kitandula, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba, pamoja na maafisa wa wizara na taasisi zake.









Share To:

Post A Comment: