WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete,

amewataka Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kusimamia mapato na malimbikizo ya madai kwa watumishi wa umma. 
Mhe.Kikwete ameyasema hayo leo Januari 15,2025 jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha 30 cha Baraza Kuu la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU).
Amesisitiza kuwa Serikali haitakubali waajiri wanaoshindwa kutekeleza matakwa ya kisheria kuhusu ushirikishaji wa mabaraza ya wafanyakazi. 
 “Ni muhimu kwa waajiri kufuata sheria na kuhakikisha wafanyakazi wanapata haki zao na Serikali itachukua hatua stahiki dhidi ya waajiri watakaoshindwa kutekeleza wajibu wao,” amesema Mhe.Kikwete
Aidha amesema kuwa  Serikali inatambua changamoto hizi na iko tayari kushirikiana na TALGWU kutafuta suluhisho la kudumu. 
“Tutaendelea kufanya kazi pamoja na vyama vya wafanyakazi ili kuhakikisha tunatatua matatizo yanayowakabili watumishi wa umma. Ufanisi wetu unatokana na ushirikiano na uwazi katika usimamizi wa fedha,” amesema Mhe. Kikwete.
Kwa upande wake  Mwenyekiti wa TALGWU Taifa ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi (TUCTA), Tumaini Nyamhokya,ameipongeza juhudi za Serikali ya awamu ya Sita chini ya  Rais Dkt.  Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutatua kero zinazowakabili watumishi wa umma.
“Serikali imesikia kilio cha muda mrefu cha watumishi waliokuwa wanalipwa mishahara kupitia mapato ya ndani ya halmashauri na kwasasa wanalipwa kupitia Mfuko Mkuu wa serikali, sambamba na kupandisha madaraja na kulipa madai yao.”amesema Bw.Nyamhokya
Awali Katibu Mkuu wa TALGWU, Rashid Mtima,ameeleza changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya umma, ikiwa ni pamoja na malipo ya fedha za likizo kutolipwa kwa wakati, matatizo katika malipo ya leseni kwa kada ya afya, na ucheleweshaji wa fedha za uhamisho.
 “Tunahitaji mfumo thabiti ambao utaweza kutatua changamoto hizi mara moja, ili watumishi wetu waweze kufanya kazi kwa ufanisi na kwa moyo mmoja,” amesema Mtima.
 Hata hivyo ameongeza kuwa mfumo wa PEPMIS umekuwa na dosari zinazohitaji marekebisho ili kuboresha utendaji wa watumishi.
Share To:

Post A Comment: