Imeelezwa kwamba hali ya amani utulivu na ushirikiano unaosimamiwa na Viongozi Wakuu wa Nchi imesaidia katika kuleta chachu kubwa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo Tanzania Bara na Tanzania Visiwani.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi ametoa kauli hiyo leo tarehe 08/01/2025 wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika ujenzi wa jengo jipya la Mahakama ya Wilaya ya Mkoani ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Amefafanua kwamba uongozi wao bora; hatuna budi kuendelea kuwaombea viongozi wetu, kila mmoja kwa dini yake ili Mwenyezi Mungu awape afya na nguvu ya kuendelea kutuongoza kwa mshikamano.
Waziri Lukuvi amesema, “chini ya uongozi wao Tanzania Bara imetulia na Tanzania Visiwani imetulia na hivyo kuwezesha haya kufanyika na kuendelea kuchochea maendeleo makubwa, mwenye macho haambiwi tazama.”
Sote ni mshahidi wa hatua kubwa za maendeleo zinazoendelea kutekelezwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia uongozi wa awamu ya nane chini ya Mhe. Daktari Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Waziri Lukuvi amesema, mafanikio ya Serikali ya awamu ya nane yanaonekana wazi katika nyanja za siasa na utawala bora, uchumi, huduma za kijamii na namna utamaduni wa watu wa Visiwa vya Zanzibar unavyoenziwa na kuheshimika wakati wote.
Aidha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imechukua hatua za makusudi kuja na mradi wa ujenzi wa jengo hili la Mahakama ya Wilaya pamoja na majengo mengine ya Mahakama za Mikoa na Wilaya kule Unguja na hapa Pemba ili kukabiliana na changamoto za miundombinu ya majengo.
“Hivyo, ujenzi wa jengo hili ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa majengo saba ambao ulipangwa kufanyika katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 alisema,” Waziri Lukuvi.
Kwa upande wake Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, Jaji Mkuu wa Zanzibar amesema Rais. Mhe. Daktari Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amewaheshimisha kwa kuwajengea majengo saba ya Mahakama za Mkoa na wilaya katika visiwa vyote vya unguja na pemba.
“Tumekusudia kusogeza huduma kwa wananchi kwa kujenga mifumo imara ya usimamizi wa haki ili kuboresha huduma zetu za mahakama kuwa za kisasa ,” alisema Mhe, Jaji, Khamis.
Naye Mhe, Valentina Katema, Mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar, amesema miundo mbinu ya majengo ya mahakama ipo katika muundo zamani hivyo kusababisha kushindwa kuendesha shughuli zake katika mazingira ya kisasa.
”Ujenzi wa majengo mapya ya Mahakama itasaidia, kupunguza msongamano wakati wa utoaji wa huduma na kusaidia wananchi kupewa huduma kwa kuendana na mahitaji ya kisasa,” alisema Mrajis.
Post A Comment: