Na John Walter -Babati

Mahakama ya Mwanzo Babati imewahukumu kifungo cha miezi miwili gerezani vijana wawili, Abubakari Semburi (18) na Abdul Hamza (18), wakazi wa Maisaka, kwa kosa la kuharibu mali ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Babati (BAWASA).

Washitakiwa hao walikutwa na hatia ya kuharibu mita za maji za BAWASA na kuziuza kama chuma chakavu katika kesi iliyowasilishwa na mlalamikaji, Sebastian Honorath, ambaye ni Meneja wa Ufundi wa BAWASA. 

Hukumu hiyo ilitolewa Januari 10, 2025, na Mheshimiwa Hakimu Kangida Kalembo, kwa mujibu wa kifungu cha 326(1) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, sura ya 16, marejeo ya mwaka 2022.

Wawili hao walikutwa na mita hizo  Desemba 24, 2024, majira ya saa saba mchana, katika maeneo ya Maisaka, mjini Babati.

Meneja wa Huduma kwa Wateja wa BAWASA, Rashidi Chalahani, amesema wamekuwa wakifuatilia kwa muda mrefu visa vya wizi wa mita za maji kutoka kwa wateja wao ambapo uchunguzi walioufanya ulipelekea kugundua mita hizo zikiwa zimeuzwa kwenye eneo la biashara ya chuma chakavu, hatua iliyosababisha kufunguliwa kwa kesi hiyo mahakamani.

Bw. Chalahani ametoa wito kwa jamii kutambua kuwa mita za maji ni mali ya umma na zinapaswa kuheshimiwa na kutunzwa. 

Aidha, amewataka wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika endapo wataona uharibifu au uhujumu wa miundombinu ya maji. 

Amesema vitendo kama hivyo vinakwamisha juhudi za serikali za kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi wote.

Hukumu hii ni onyo kwa wale wanaojihusisha na uharibifu wa miundombinu ya umma, huku ikisisitiza umuhimu wa kushirikiana katika kulinda rasilimali za taifa.

Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Post A Comment: