MKUU wa wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Mwanahamisi Munkunda amewataka wawekezaji kwenda kuwekeza katika wilaya hiyo kwani tatizo la maji ambalo lilikuwa kero kwao limeshapatiwa ufumbuzi wa kudumu.


Alitoa kauli hiyo jana alipofanya kikao na Wadau wa maji na menejimenti ya Mamlaka ya Maji Same Mwanga (Samwasa) mara baada ya kutembelea na kujionea mradi wa maji Mwanga - Same - Korogwe ambao awamu ya kwanza imeshakamilika na maji yanatoka katika wilaya ya Mwanga na Same.

Alisema kuwa, awali wawekezaji walikuwa wakishindwa kuwekeza katika wilaya hiyo kutokana na tatizo la maji lakini kwa sasa kupitia serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweza kukamilisha mradi huo.

"Tunatambua wawekezaji wengi walikuwa wakikataa kuja kuwekeza katika wilaya yetu kutokana na tatizo la maji tulilokuwa nalo lakini serikali imeonyesha kwa vitendo kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi wake ambapo kwa sasa tunapata maji masaa 24" Alisema Mwanahamisi.

Alisema kuwa, mradi huo umeliliwa na wananchi kwa muda mrefu lakini Dkt. Samia amekuja kuumaliza na kutatua kiu ya Wanamwanga ambapo kwa sasa wanayo maji ya kutosha.

Mkuu huyo alidai kuwa, lengo la mradi huo ni kuifungua wilaya ya Mwanga kiuchumi na kimaendeleo na kuwataka kuwa walinzi wa mradi huo ili uweze kudumu muda mrefu.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa wilaya amewataka Watumishi wa Mamlaka ya maji Samwasa kubadilisha utendaji kazi na kuachana kufanya kazi kwa mazoea ili lengo la serikali na kuwahudumia wananchi wake liweze kutimia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji Samwasa, Mhandisi Rashid Mwinjuma alisema kuwa, uhitaji wa maji kwa wilaya ya Mwanga na Same ni lita za ujazo milioni 8 kwa siku huku mradi huo ukiweza kuzalisha lita za ujazo milioni 55.5 kwa siku hivyo maji yapo ya kutosha.

Mhandisi Mwinjuma alisema kuwa, kwa sasa Mamlaka hiyo inazidai taasisi za serikali na watu binafsi milioni 149.23 kwa Mwanga na milioni 132.22 kwa Same ambapo amehimiza wananchi kuendelea kulipa Ankara zao pamoja na madeni.

Alisema kuwa, kwa sasa Mamlaka hiyo inakabiliwa na changamoto ya uchelewaji wa vifaa kama mabomba kea ajili ya maunganisho ya maji kwenye mtandao wa mradi, uhaba wa fedha inayopelekea kutomudu gharama za ujenzi wa miradi na uendeshaji.

"T inakabiliwa na changamoto ya baadhi ya wateja kutolipa Ankara zao kwa wakati ambapo kwa sasa tunadai zaidi ya milioni 281 lakini pia upotevu wa maji mkubwa kutokana na uchakavu wa miundombinu" Alisema Mhandisi Mwinjuma.






Share To:

Post A Comment: