Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka watumishi wa umma wanaohudumu chini ya ofisi yake kutojiusisha na shughuli za siasa kama ambavyo Sheria, Kanuni na Taratibu za utumishi wa umma zinavyoelekeza.
Waziri Mchengerwa ametoa maelekezo hayo leo Januari 22, 2025, wakati akijibu hoja za baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inayoendelea na vikao vyake vya kawaida jijini Dodoma chini ya mwenyekiti wake Mhe. Justine Nyamoga.
“Kwa mujibu wa Kanuni F.21 (b) ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma toleo la Mwaka 2009 mtumishi wa umma harusiwi kujihusisha na shughuli za kisiasa wakati akiendelea kutekeleza majukumu yake ya kiutumishi, hivyo ofisi yangu haitosita kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wote wanaokiuka kanuni hiyo,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Mhe. Mchengerwa amewaelezea wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuwa, Ofisi yake haiungi mkono watumishi wanaoacha kutekeleza majukumu yao ya msingi na badala yake wanajishughulisha na masuala ya kisiasa ambayo yanaathiri utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, uwepo wa baadhi ya watumishi wanaotumia rasilimali za Serikali kufanya shughuli zao za kisiasa ni jambo ambalo hawezi kulifumbia macho na kueleza kuwa tayari ameshatoa maelekezo kwa Katibu Mkuu OR-TAMISEMI kufuatilia kwa ukaribu madai hayo ili hatua stahiki zichukuliwe.
“Taratibu ziko wazi kama kuna mtumishi anahitaji kuingia kwenye siasa anapaswa kuzingatia taratibu za kiutumishi ikiwepo kumfahamisha mwajiri wake na kwa baadhi ya nyadhifa mtumishi anapaswa kujiudhuru ili aingie moja kwa moja kwenye siasa, hivyo ninashauri watumishi wa umma kuzingatia Kanuni, Sheria, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Aidha, Waziri Mchengerwa katika mahojiano yake na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya OR-TAMISEMI, amesisitiza kuwa Watumishi wa Umma wanapaswa kuwa waadilifu kwa kutojihusisha na shughuli za kisiasa kama ambavyo Kanuni F.21 (b) ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma toleo la Mwaka 2009 inavyoelelekeza.
Post A Comment: