Na Farida Ramadhani, WF - Dodoma.
Serikali imezisisitiza Wizara zote na taasisi zake kuendelea kutenga fedha kwenye mafungu yao kwa ajili ya kutoa elimu kwa umma kuhusu utekelezaji na mafanikio ya shughuli na miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mhe. Janeth Maurice Massaburi aliyetaka kujua mpango wa Serikali kutenga bajeti ya elimu kwa umma kwa masuala mbalimbali yanayotarajiwa kutekelezwa nchini.
Mhe. Chande alisema Serikali inatambua umuhimu wa utoaji wa elimu kwa umma kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo na kijamii.
“Katika kuhakikisha kuwa jamii inapata uelewa wa kazi mbalimbali zinazotekelezwa na Serikali, Wizara zote na Taasisi zake zinasisitizwa kutenga fedha kwenye mafungu yao kwa ajili ya kutoa elimu kwa umma kuhusu utekelezaji na mafanikio ya shughuli na miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali”, alibainisha Mhe. Chande.
Aliongeza kuwa kwa mujibu wa muundo na mgawanyo wa majukumu ya Serikali, jukumu hili linatekelezwa na Idara ya Habari Maelezo, Wizara ya Habari, Michezo, Utamaduni na Sanaa pamoja na Vitengo vya Mawasiliano Serikalini katika Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi zote za Umma.
Post A Comment: