Na, Egidia Vedasto Arusha.
Wanawake Jijini Arusha wamenufaika na mafunzo ya uongozi wa mabadiliko kutoka kwa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wanawake (UN Women) kwa ushirikiano na Serikali ya Finland ili waweze kuleta mabadiliko chanya katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Wanawake (UN Women) Hodan Addou amezungumzia masuala ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wananwake katika masuala mbalimbali ikiwemo uchumi na siasa.
Amesema kuwa (UN Women) imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha kuwa wananwake wanapata nafasi sawa katika sekta zote za maendeleo na kusisitiza umuhimu wa kushirikiana katika mipango ya maendeleo jumuishi inayozingatia mahitaji ya wanawake vijijini na wale walioko mazingira magumu.
"Uwezeshaji wa wananwake si tu suala la haki za binadamu bali ni msingi wa maendeleo endelevu, na tunafurahi kuona Mkoa wa Arusha ukichukua hatua madhubuti katika kusimamia usawa wa kijinsia" ameeleza Addou.
Kwa upande wake Muwezeshaji wa mafunzo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Prof. Bernadetha Killian amesema mafunzo hayo yanawalenga wanawake viongozi ngazi za serikali za mitaa, (TAMISEMI) Madiwani waliochaguliwa na wale viti maalum, wenyeviti serikali za mitaa, wenyeviti serikali vijiji na wenyeviti majukwaa mbalimbali.
Vilevile amewasisitiza wanawake waliopata mafunzo kuhudhuria mafunzo hayo kwa siku zote zilizopangwa, kujiamini na kutunza vitabu vya kumbukumbu.
"Mradi huu ni wa mwaka mmoja, umeanza Oktoba 2024 na utakamilika Septemba 2025 kwa ufadhili wa (Un Women) kwa ushirikiano wa Serikali za mitaa na mkoa kupitia kwa Maafisa maendeleo ya jamii lwa ajili ya kutafuta walengwa stahiki, nno furaha yetu kwamba tumefanikisha hilo" amebainisha Prof. Bernadetha.
Hata hivyo mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo na mwenyekiti wa jukwaa la wanawake kata ya Muriet Miriam Mbise amewataka wanawake kuacha woga katika masuala ya siasa na uchumi bali wathubutu kupaza sauti ili kupigania haki na kutimiza ndoto zao.
"Wananwake wa Kaskazini tuache woga, tujione tunafaa maana sisi ni viongozi kuanzia katika ngazi za familia zetu, tena tuwaze kugombea nafasi za juu" amesema Miriam.
Post A Comment: