WANANCHI wa kijiji cha Liweta Halmashauri ya wilaya Songea mkoani Ruvuma,wameishukuru Wakala wa barabara za vijijini na mijini(TARURA)kwa kuwajengea daraja la kudumu katika mto Liweta linalounganisha kijiji hicho na Masuku na maeneo yao ya kilimo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema,awali walikuwa wakipata shida kubwa kupitia katika eneo hilo hasa wakati wa masika wanapotaka kwenda mashambani na vijiji vya jirani kutokana na kukosekana kwa kivuko hali iliyochangia kuwarudisha nyuma kiuchumi.
Micheal William alisema,kabla ya daraja hilo walitumia siku tatu hadi nne kusubiri maji yapungue ndipo waendelee na safari kwenda kitongoji cha Litapatile na kijiji cha Masuku,lakini sasa hakuna tena changamoto hiyo baada ya kujengewa daraja la kudumu.
Hata hivyo,ameiomba Serikali kuendelea kuwasaidia kwa kuboresha barabara hiyo hadi maeneo ya Litapatile ambako kuna uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na biashara ili wakulima waweze kuwa na uhakika wa kusafiri mazao yao.
“Wapo ndugu zetu waliofariki Dunia kwa kusombwa na maji walipokuwa wakijaribu kuvuka kipindi cha mvua kutokana na kukosekana kwa daraja,lakini sasa baada ya kujengwa kwa daraja hili ni furaha na neema kubwa kwetu”alisema.
Aidha alisema,awali hali ilikuwa mbaya zaidi kwa watoto wanaoishi mashambani kwani mto huo unapojaa maji walikaa muda mrefu kusubiri hadi maji yapungue ili waweze kwenda shule hivyo kukosa baadhi ya vipindi vya masomo.
Mkazi mwingine wa kijiji cha Masuku Malaika Komba alisema,miaka ya nyuma walikuwa kwenye mateso makubwa kupita katika eneo hilo kutokana na kujaa maji mengi na pindi walipotaka kwenda upande mwingine walitumia muda mrefu.
“tunaishukuru sana Serikali kwa kutuangalia kwa jicho la huruma na kutujengea daraja katika eneo hilo,hapa tumepoteza mazao yetu kwa kusombwa na maji pindi tulipotaka kuvuka kwenda kijijini kutafuta masoko”alisema Komba.
Kaimu meneja wa Tarura wilaya ya Songea Godfrey Mngale alisema,Serikali imetumia Sh.milioni 449 kujenga daraja na kufanya upanuzi wa barabara hiyo ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa mazao kutoka shambani kwenda sokoni.
Alisema kuwa,daraja hilo ni muhimu katika kurahisisha mawasiliano na itarahisisha kufungua maendeleo ya wananchi wa kijiji cha Liweta,Masuku na Halmashauri ya wilaya Songea ambao walikuwa na uhitaji mkubwa wa daraja la kudumu.
Mngale,ametoa wito kwa wananchi kulilinda miundombinu ya daraja kwa kutojihusisha na vitendo vya kuchimba mchanga chini ya daraja,kuiba alama za barabarani na kuacha kupitisha mifugo juu ya daraja kwani Serikali imetumia gharama kubwa kujenga daraja na barabara.
Kwa upande wake meneja wa TARURA mkoa wa Ruvuma Silvester Chinengo alisema,daraja la Liweta ni moja ya miradi ya kuondoa vikwazo vya usafirishaji katika mkoa wa Ruvuma na daraja lina upana wa mita 20 na njia nne za kupitisha maji.
Chinengo alisema,daraja la Liweta linaunganisha kijiji cha Liweta na Masuku na kabla ya kujengwa wananchi walikuwa wanapata adha kubwa kupita kwenye maji na msimu wa kilimo walishindwa kwenda upande wa pili kwa ajili ya kuendelea na shughuli zao za uzalishaji.
“kwa hiyo Serikali kupitia mradi wa kuondoa vikwazo vya usafirishaji unaofadhiliwa na Benki ya Dunia ndiyo uliofanikisha ujenzi wa daraja hili na kwa sasa wananchi wanafurahia huduma inayotolewa na Serikali yao ya awamu ya sita”alisema Chinengo.
Chinengo,ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha zilizotumika kujenga daraja hilo ambalo limewezesha kuondoa kikwazo cha usafirishaji kilichowatesa wananchi wa maeneo hayo kwa muda mrefu.
muonekano wa daraja la Liweta-Masuku Halamshauri ya wilaya Songea linalojengwa na wakala wa barabara za vijijini na mijini Tarura ambapo ujenzi wake umekamilika kwa zaidi ya asilimia 98.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Silvester Chinengo kushoto na kaimu meneja wa TARURA Wilaya ya Songea Godfrey Mngale wakikagua ujenzi wa daraja la Liweta-Masuku jana.
Kaimu meneja wa TARURA wilaya ya Songea Mhandisi Godfrey Mngale wa pili kulia na baadhi ya Waandishi wa habari wakikagua ujenzi wa daraja la Liweta-Masuku katika Halmashauri ya wilaya Songea mkoani Ruvuma.
Post A Comment: