Na Denis Chambi, Tanga.

BARAZA la madiwani wa  Halmashauri  ya Jiji la Tanga limevitaka viwanda vya Tanga Cement  ,Pwani Cement pamoja na Kilimanjaro Cement  kulipa fedha za tozo   zaidi ya shilingi Milion 4 wanazodaiwa fedha ambazo zinatajwa kuchangia halmashauri hiyo kushuka katika makusanyo yake ya mapato kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la madiwani  cha pili cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025 Mstahiki  Meya wa Halmashauri hiyo Abdurlahman Shillow ameeleza kuwa  tayari wameshafanya vikao vya pamoja na viwanda hivyo kwaajili ya kutekeleza makubaliano ya kulipa fedha hizo ambazo zitachangia mapato ya halmashauri kuongezeka.

"Tumekuwa nyuma kidogo kwenye suala la mapato mpaka mwezi December 2024 lakini hii imesababishwa na wenzetu wa viwanda vya madini vya Tanga Cement,Kilimanjaro Cement na Pwani Cement ambao walikuwa wamegoma  kutoa fedha za  tozo ya madini"

"Tayari   tumefanya nao vikao kwa muda   pamoja na kamati ya fedha na Mkuu wa mkoa kuna makubaliano ambayo tumeyafikia tunategemea tuanze kuona mabadiliko hivyo watu wa Tanga wasije wakasema kuwa halmashauri yetu inaanguka katika makusanyo tunakwenda  vizuri hawa wenzetu ndio waliokuwa wakituvuta  tunaamini kwamba wakituingizia fedha hizo ambazo tunadai halmashauri itakaa kwenye sehemu yake" alisema Shillow.

Katika hatua nyingine Baraza hilo limemtaka Mkurugenzi na wataalamu wake wa mazingira kutatua changamoto ya vumbi inayosababishwa na viwanda vilivyopo katika eneo la kata ya Maweni ambapo wananchi waishio katika maeneo hayo wamekuwa wakiathirika kwa muda mrefu.

Kufwatia maelekezo yaliyotolewa na Baraza hilo   diwani wa kata ya Maweni Joseph Colvas amesema hatua hiyo itakwenda kuondoa changamoto  iliuodumu kwa muda mrefu.

"Kata yetu imebarikiwa kuwa na viwanda vingi katika halmashauri yetu ya Jiji la Tanga lakini tuna tatizo kubwa la vumbi kwa wakazi wa kata yetu hii imekuwa ni kero ya muda mrefu ninaamini itakwenda kupatikana tiba ya kudumu" alisema Colvas.

Aidha Baraza hilo pia limempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kipitishwa na mkutano mkuu wa chama cha Mapinduzi 'CCM' kuwa mgombea wa kiti cha urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 akiwa pamoja na mgombea Mwenza Balozi Emmanuel Nchimbi.
Share To:

Post A Comment: