Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla amewataka vijana kuendeleza umoja na mshikamano pamoja na kuwa na dhamira njema ya kuijenga nchi ili kila mmoja  aweze kunufaika na matunda ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.

Akizungumza na Vijana wa Umoja wa Vijana wa CCM Zanzibar ( UVCCM ) kwa niaba ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati wa Uzinduzi wa Matembezi ya Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar Katika Uwanja wa Mpira wa Tumaini Mkwajuni, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema katika kujenga Nchi yenye maendeleo ni lazima kuwepo na misingi Imara itakayolisaidia Taifa kufikia malengo yake, ni lazima jamii iweze kuepukana na vitendo viovu vya dhulma, chuki, rushwa na ufisadi kwa mustakbali mwema wa vizazi  vya sasa na  baadae.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema vijana watakaposhikamana vizuri na kusaidiana katika kutafuta na kutengeneza ajira wanaweza kutatua kwa kiwango kikubwa changamoto mbali mbali za kimaendelo zinazoikumba jamii katika kufikia Mapinduzi ya kiuchumi na kimaendelo.

Sambamba na hayo amefahamisha kuwa Serikali imedhamiria kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa makundi yote ya vijana kwa lengo la kuhakikisha inawapatia fursa za ajira kwa namna iliyo bora na sahihi kwa mujibu wa taratibu za nchi ikiwa ndio fikra na falsafa za muasisi wa Mapinduzi matukufu ya Mwaka 1964.

Mhe Hemed amesema kutokana na mchango mkubwa unaotolewa na vijana katika kujenga jamii yenye maendeleo amewahakikishia kuwapatia mashirikiano na kuwapa kipao mbele katika kukikuza Chama Cha Mapinduzi na Taifa kwa ujumla.

Nae Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa Comred MOHAMED ALI KAWAIDA amesema watahakikisha watayatumia matembezi hayo kwa kuwahamasisha Vijana na wananchi wote kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura ili Chama cha Mapinduzi kiweze kushinda kwa kishindo  katika uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2025 ili  CCM iendelea kushika Dola.

Mwenyekiti Kawaida amesema kuwa Vijana watahakikisha wanalinda na kudumisha Umoja, Amani na Mshikamano ambao ndio fikra na falsafa ya muasisi wa Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ambayo ndio chachu ya maendeleo nchini .

Kwa upwnde wake Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM anaefanyia kazi zake Zanzibar Ndugu ABDI MAHMOUD ABDI amesema Matembezi hayo yatakayojumuisha vijana zaidi ya Elfu  nne(4000) yana lengo la kuadhimisha Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar amabayo yameifanya zanzibar kuwa nchi yenye na Amani na Utulivu.

ABDI amesema kupitia Matembezi hayo vijana watatoa elimu kwa wananchi wa Zanzibar juu ya umuhimu wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ambayo yamemkomboa Mzanzibari kutoka katika madhila ya Wakoloni pamoja na kusambaza kauli zenye kuhamasisha Amani na Upendo kwa maendeleo endelevu ya Zanzibar.

Amefahamisha kuwa Vina wa UVCCM wameandaa matembezi hayo kuudhihirishia Umma wa Kitanzania na Dunia kwa ujumla kuwa vijana wapo tayari kuyalinda, kuyaenzi na kuyatetea Mapinduzi kwa nguvu na gharama yoyote ile na hawatokuwa tayari kuchokozeka kwa kauli za wapinzani zisizo na mustakbali mwema wa Taifa.

Matembezi hayo yaliyozinduliwa leo yatapita katika Mikoa  na Wilaya zote za Unguja na Pemba ambayo yanatarajiwa kufikia kikomo Januari 10, 2025 katika Mkoa wa Kaskazini Pemba na kufungwa rasmi na Mwenyekiti wa CCM Taifa ambae pia ni Rais wa Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Mjumbe wa  Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla akimkabidhi Bendera  Kiongozi wa Matembezi ya Umoja wa Vijana wa CCM Zanzibar ( UVCCM )Komred Juma Usonge kwa niaba ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi nikiashiria Uzinduzi wa Matembezi ya Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar Katika Uwanja wa Mpira wa Tumaini Mkwajuni, Mkoa wa Kaskazini Unguja na kupitia katika Wilaya na Mikoa yote ya Unguja na Pemba na kufikia tamati tarehe 10 Januari 2025 katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.




 
Share To:

Post A Comment: