Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti SaoHill PCO Tebby Yoramu akizungumza na watalii ambao wametembelea shamba hiyo kwa ajili ya utalii wa ndani
Watalii wakifurahia utalii ndani ya shamba la miti Sao Hill lililopo wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.
Watalii wakifurahia utalii ndani ya shamba la miti Sao Hill lililopo wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.


Na Fredy Mgunda, Iringa.

Kundi la  wadau wa utalii kutoka katika Mkoa wa Dar es Salaam wametembelea Shamba la Miti Saohill liliopo Mkoani Iringa, Mafinga linalosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ambapo wameweza kuzunguka na kufanya shughuli mbalimbali za utalii.


Miongoni mwa shuguli walizozifanya ni utalii wa kuendesha baiskeli (Cycling) na kuweka kambi ya kitalii (Camping) katika maeneo tofauti yaliyo ndani ikiwa ni pamoja na eneo la msitu wa kupandwa lililopo karibu na Mto Ruaha mdogo wenye eneo oevu na la kuvutia, Hifadhi ya Msitu wa Asili Kigogo (Kigogo Nature Forest Reserve) pamoja na Bwawa la Ngwazi lililopo pia ndani ya Shamba la Miti SaoHill.


Aidha waliweza kujionea maporomoko ya maji, wanyama, maua, aina tofauti tofauti za ndege na wadudu wanaopatikana msituni, shughuli za uvuvi, pamoja, kuzama kwa jua (Sunset) na maeneo ya uwanda wa juu wa ardhi (View points) yanayopatikana katika katika maeneo ya msitu wa SaoHill.


Akizungumza muandaaji wa safari hiyo na mdau wa masuala ya utalii wa misitu Bw. Mathias David Manyanya ametoa pongezi kwa Kamishna wa Uhifadhi -TFS Prof. Dos Santos Silayo, kwa kuwa TFS kupitia Shamba la Miti SaoHill inafanya kazi kubwa ya uhifadhi wa misitu na vyanzo vya maji katika maeneo mengi yaliyohifadhiwa ambayo yamepelekea kufanya maeneo hayo kuvutia kwa utalii na shuguli mbalimbali za utafiti.


Amesema kuwa ni muda sasa wa watanzania wengine kuelewa kuwa ndani ya misitu ya kupandwa kuna shughuli za utalii pia zinazoweza kufanyika ambazo zinachangiwa na uwepo wa misitu ya asili ndani yake hivyo ni muhimu kubadili mtazamo na kuanza utalii katika hifadhi za misitu ya kupandwa na asili

"Nilivyofika mara ya kwanza sikutegemea nitakutana na mazingira mazuri yaliyojificha katika eneo hili la Shamba la Miti SaoHill  kwani ni eneo lenye uzuri wa kipekee ,nimeona maporomoko, wanyama na ndege mbalimbali, nipende kuwaasa watanzania wenzangu waje kutembelea maeneo ya ndani ya nchi yetu bila shaka watafurahi pia" John Kinyaki-Mfanyabiashara na Mdau wa Utalii wa Misitu.


"Kwa kifupi naweza kusema Tanzania tumebarikiwa, nimefika Shamba la Miti SaoHill na kuna vivutio vingi sana hususani maeneo ya kuweka kambi ikiwepo eneo la bwawa na misitu ya asili yenye wanyama pia, ni vyema watanzania kufika katika eneo hili kufanya utalii na kuunga juhudi za serikali ya awamu ya sita chini ya Mama yetu Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan katika kukuza utalii" Abiath Kivewo-Mtalii


"Watu wengi walioko katika maeneo mengine  hawajui uzuri uliopo katika hifadhi za misitu, maeneo haya ukiwaonyesha watu wengi watakwambia hapa sio Tanzania hivyo ni muda sasa na wao kufika katika maeneo haya na kuona tofauti ya kuvutia katika hifadhi za misitu"  Deogratius Balthazar- Mtalii na Mdau wa Masuala ya Utalii.


Kwa ujumla wao wametoa pongezi kwa Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti SaoHill PCO Tebby Yoramu kwa mapokezi mazuri na muongozo mzuri walioupata toka wa wahifadhi wengine tangu wamefika mpaka kumaliza kwa matembezi hayo.


Kwa upande wake Mhifadhi anayehusika na Utalii katika Shamba la Miti SaoHill Bob Matunda amesema kuwa watalii hao wameleta chachu, hivyo kupitia wao shughuli za kiutalii katika Shamba zitaongeza hamasa ya wadau wengine kuja kutalii na hata kufanya uwekezaji kutokana na uzuri wa maeneo mengi ya hifadhi.


Shamba la miti Saohill linahusisha maeneo ya misitu wa kupandwa, misitu ya asili na vyanzo vya maji ambapo ndani yake kuna maporomoko ya maji, maeneo ya uwanda wa juu, maeneo uevu, wanyama, wadudu na mimea ya aina mbalimbali ambavyo ni fursa kubwa ya shughuli za utalii na mafunzo.

Share To:

mwangaza wa hbari

Post A Comment: