Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo, ameweka wazi mikakati yake ya kushirikisha makundi mbalimbali katika kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia. 

Akizungumza Jumamosi, Januari 11, 2025, katika hafla maalumu ya uhamasishaji wa nishati safi kwa viongozi wa dini ya Kiislam jijini Arusha, Gambo ameelezea jinsi walivyolenga makundi kama walimu, mama lishe, na walemavu ili kuhakikisha ujumbe wa nishati safi unafikia jamii kwa kina.  

“Tumewashirikisha walimu 5,000 bila kujali kama ni wa serikali au wa sekta binafsi. Tunaamini ukimuelimisha mwalimu, umeielimisha jamii nzima kwa sababu mwalimu ana ushawishi mkubwa na huwasiliana na watu wengi kila siku,” amesema Gambo.  

Ameongeza kuwa walimu hao hawakupewa elimu peke yake, bali pia walipewa vifaa vya kutumia kama mitungi ya gesi. 

“Huu mtungi si zawadi, bali ni kitendea kazi. Ukifundishwa kwa vitendo na tayari unacho kitu cha kutumia, ni rahisi zaidi kwao kuhamasisha wengine. Hata hivyo, hatumaanishi kwamba hawawezi kununua mitungi, lakini tunatoa mitungi hii kama chachu ya kuhamasisha kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan,” ameongeza.  

Hafla hiyo imefanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) na ilihudhuriwa na viongozi wa serikali za mitaa, wajumbe wa Jumuiya ya Maridhiano, viongozi kutoka Wizara ya Nishati, watendaji wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), masheikh kutoka taasisi mbalimbali za dini ya Kiislamu, na wadau wa nishati safi nchini.








Share To:

Post A Comment: