Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeshiriki kwa umahiri katika Mkutano wa Africa Energy Summit 2025 unaoendelea katika Ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam, ukihudhuriwa na viongozi wa mataifa zaidi ya 25 barani Afrika, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kutangaza utalii wa ikolojia, malikale, na bidhaa za nyuki.

Mkutano huo, uliofunguliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, umelenga kujadili upanuzi wa miundombinu ya nishati na kuvutia wawekezaji katika vyanzo mbadala vya nishati kama vile jua, upepo, na gesi asilia.

Akizungumza katika maonyesho ya TFS kwenye mkutano huo unaoongozwa na Rais mwenyeji, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jana Januari 27, 2025, Mkuu wa Kitengo cha Uhamasishaji Utalii, Anna Lauwo, alisema kuwa ushiriki wa TFS ni fursa muhimu ya kuonyesha umuhimu wa rasilimali za misitu katika maendeleo endelevu, pamoja na kutangaza utalii wa ikolojia na malikale zinazosimamiwa na wakala huo.

“Kupitia mkutano huu, tumewahamasisha washiriki wa ndani na nje ya nchi kufahamu zaidi kuhusu vivutio vya kipekee vya utalii kama Maporomoko ya Hululu, Msitu wa Amani, Hifadhi ya Pugu Kazimzumbwi, na Hifadhi ya Uluguru. Pia, tumeeleza nafasi ya urithi wa kihistoria unaopatikana kwenye maeneo haya, ambao ni kivutio kikubwa kwa watalii,” alisema Lauwo.

Aidha, Lauwo alibainisha kuwa TFS imetumia jukwaa hilo kutangaza Misitu Honey, asali bora inayozalishwa kwa viwango vya kimataifa, huku ikiainisha nafasi ya ufugaji nyuki endelevu katika kukuza ajira na kulinda mazingira. “Washiriki wamepata fursa ya kuonja na kujifunza zaidi kuhusu bidhaa zetu za nyuki, na tumehimiza uwekezaji zaidi katika sekta hii muhimu,” aliongeza.

Mhifadhi Lauwo pia alisema kuwa TFS imeonyesha wazi kuwa sekta ya misitu inaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi wa kijani na kuimarisha utalii endelevu.

Alisisitiza kuwa ushiriki wa Tanzania kwenye mkutano huu siyo tu fursa ya sekta ya nishati, bali pia ni jukwaa la kuonyesha juhudi za taifa katika kulinda maliasili, kukuza utalii, na kuhakikisha maendeleo endelevu.

“Tunawahimiza washiriki wote kutembelea misitu na hifadhi mbalimbali tunazosimamia ili kujionea uzuri wa rasilimali zetu, kujifunza kuhusu uhifadhi wa mazingira, na kushiriki katika kukuza utalii wa ikolojia hapa nchini,” alihitimisha Lauwo.

Mkutano wa Africa Energy Summit 2025 unalenga kujadili na kuimarisha maendeleo ya sekta ya nishati, kwa kutilia mkazo upanuzi wa upatikanaji wa umeme, uboreshaji wa miundombinu ya nishati, na kutafuta suluhisho za changamoto zinazokwamisha ukuaji wa sekta hiyo.

Pia, mkutano huu unalenga kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi katika sekta ya nishati, hususan kwenye vyanzo mbadala kama vile nishati ya jua, upepo, na gesi asilia.






Share To:

Post A Comment: