Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Mufindi wamepanda jumla ya miti elfu tano (5000) katika Shule ya Sekondari Mufindi iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi na Shule ya Sekondari Saohill iliyopo Halmashauri ya Mji Mafinga leo tarehe 27 Januari 2025 ikiwa ni uzinduzi wa upandaji wa miti kiwilaya.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa zoezi hilo mgemi rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mhe Dkt Linda Salekwa amewapongeza TFS na TAKUKURU kwa kuratibu zoezi hilo ikiwa ni hatua ya kuendelea kutunza mazingira kwa kupanda miti.
Amesema kuwa Wilaya ya Mufindi imekuwa ikipata mvua nyingi kila mwaka hali inayochangiwa na uwepo wa misitu na hivyo kuwataka wananchi kutumia mvua zinazoendelea kunyesha kwa ajili ya upandaji wa miti katika maeneo yao.
Sambamba na hayo amewaasa viongozi wa Halmaushauri ya Wilaya ya Mufindi, Halmashauri ya Mji Mafinga, walimu na wanafunzi kuhakikisha miti iliyopandwa katika shule hizo inatunzwa ili iweze kukua vizuri na kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Mufindi Bw. Abdull Abdarahman ameishukuru TFS kwa kuwezesha upatikanaji wa miti hiyo (5000) kwa ajili ya kupanda katika shule hiyo na kuwafanya kuwa sehemu muhimu ya utunzaji wa mazingira.
Aidha ameongeza kuwa kupitia kampemi hiyo ya upandaji wa miti imesaidia pia kuwafikia makundi mbalimbali zikiwepo shule na wananchi wengine kwa ajili ya kutoa elimu inayohusiana na masuala ya rushwa.
Naye msaidizi wa Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti SaoHill upande wa uendelezaji wa Shamba SCO. Said Singano amesema kuwa TFS itaendelea kutoa ushirikiano katika shuguli zote uhifadhi ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu ya upandaji na utunzaji wa miti katika maeneo mbalimbali na kuwaasa pia wananchi kuendelea kutumia mvua zinazonyesha katika upandaji wa miti
Upandaji huo wa miti umefanyika kwa kushirikiana na wadau wengine wa mazingira katika Wilaya ya Mufindi huku malengo ya upandaji wa miti kwa mwaka 2025 ikiwa ni jumla ya miti milioni ishirini na tano.
Post A Comment: