Kamati ya kudumu ya Bunge ya TAMISEMI ikiongozwa na mwenyekiti wake Mhe. Justin Lazaro Nyamoga imeishauri Wakala wa barabara za Mijini na Vijijini - TARURA mkoani Rukwa kuweka taa za barabara kwa kutumia fedha zinazobaki kwenye miradi iliyokamilika badala ya kusubiri fedha za bajeti mpya ya Serikali.
Mhe. Nyamoga ametoa ushauri huo, wakati wa kikao cha majumuisho cha Kamati hiyo katika mkoa wa Rukwa mara baada ya kukamilisha ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Ofisi ya Rais - TAMISEMI mkoani humo.
“Kuna barababara tumeikagua hapa Sumbawanga na kuilekekezaTARURA kuanza kuweka taa za barabarani kwa kutumia fedha zilizobaki badala ya kusubiria fedha za bajeti mpya ya mwaka wa fedha 2025/26, kwani kwenye bajeti zao inaonekana kuna fedha kidogo zimebaki,” Mhe. Nyamoga amesisitiza.
Akizungumzia utoaji wa huduma bora za Afya Msingi kwa wananchi, Mhe. Nyamoga ameishauri Manispaa ya Sumbawanga kutumia mapato ya ndani kukarabati majengo ya zamani ili yawe na miundombinu bora itakayowawezesha watumishi wa kada ya afya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Akipokea maelekezo hayo ya Kamati, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Zainab Katimba ameahidi kusimamia vema utekelezaji wa maelekezo hayo ili majengo yakarabatiwe na yatumike kutoa huduma bora za afya msingi kwa wananchi.
Kamati ya kudumu ya Bunge ya TAMISEMI imehitimisha ziara ya kikazi mkoani Rukwa kwa kutembelea na kukagua mradi wa elimu wilayani Nkasi uliojengwa na Serikali kupitia mradi wa BOOST, miradi ya afya wilayani Nkasi, Sumbawanga na Manispaa ya Sumbawanga pamoja na mradi wa barabara katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga.
Post A Comment: