Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) kimewataka wawekezaji wa Kitanzania kusajili miradi yao katika kituo hicho ili kufaidika na fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali, ikiwa ni pamoja na msamaha wa ushuru wa mitambo na bidhaa maalum zinazoagizwa kutoka nje. Wito huu umetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Uwekezaji Nchini, Dkt. Binilith Mahenge, alipotembelea wawekezaji waliowekeza mkoani Simiyu.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Mahenge alisema kuwa TIC ina utaratibu wa kusajili miradi ya Watanzania wenye mtaji wa kuanzia dola 50,000. Pia alieleza kuwa kwa miradi iliyosajiliwa, TIC hutoa usaidizi katika kutatua changamoto mbalimbali na kuhakikisha wanachama wanapata manufaa yanayostahili kutokana na uwekezaji wao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri, aliwapongeza wawekezaji waliowekeza katika sekta ya viwanda, hususan Kiwanda cha Kuchakata Pamba cha Alliance kilichopo mkoani Simiyu. Teri alieleza kuwa kiwanda hicho kimechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la ajira kwa kuongeza nafasi za ajira kwa wananchi wa eneo hilo. Aidha, aliwasihi wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda nchini kuhakikisha wanatumia TIC kusajili biashara na miradi yao kwa urahisi.

Meneja wa Kiwanda cha Kuchakata Pamba cha Alliance, Boaz Ogola, alisema kuwa mazingira ya uwekezaji kwa sasa ni rafiki, na kwamba hatua za kupata leseni na vibali vya biashara zimeboreshwa, hali ambayo imepunguza vikwazo vilivyokuwepo awali.

Naye, Kaimu Mkuu wa Idara ya Uchumi na Uzalishaji wa Mkoa wa Simiyu, Juma Kazula, alisema kuwa hali ya uwekezaji mkoani humo ni nzuri, kwani halmashauri zote za mkoa zimepanga na kutenga maeneo maalum kwa ajili ya uwekezaji. Hii imechangia kuvutia wawekezaji na kuimarisha shughuli za kiuchumi katika mkoa wa Simiyu.

Share To:

JOEL MADUKA

Post A Comment: