Na Farida Mangube, Morogoro
Jumla ya wasichana 10,239 waliokuwa wamekatisha masomo wamenufaika na Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP), unaotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (MoEST) na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kwa kushirikiana na Benki ya Dunia.
Akizungumza mjini Morogoro, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema lengo kuu la SEQUIP ni kuimarisha ubora wa elimu kwa wanafunzi walioshindwa kuendelea na masomo yao, hususani wasichana waliopata changamoto kama ujauzito, ndoa za utotoni, au mazingira magumu.
"Mpango huu umelenga kuwafikia wasichana 12,000 wenye umri wa miaka 13 hadi 21. Pia tunajipanga kuwarejesha wavulana wengi zaidi mashuleni kabla na hata baada ya mradi huu kumalizika," ameeleza Waziri Mkenda
Aliongeza kuwa kupitia SEQUIP, wasichana wapatao 351 wamesajiliwa kujiunga na kidato cha tano, huku 218 wakijiunga na vyuo vya kati.
Silvia Diskon ni mmoja wa wanafunzi waliopata habati ya kurudi shule kupitia mpango huo amesema hakubahatika kumaliza masomo yake kutokana na changamoto za kifamilia hivyo anaishukuru serikali kupitia SEQUIP ataweza kutimiza ndoto yake ya kuwa mwalimu baada ya kurudi shule.
Kamishna wa Elimu, Dk. Lyabwene Mtahabwa, amesema kuwa walaka wa Serikali wa mwaka 2021 kuhusu urejeshwaji wa wanafunzi mashuleni umechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha lengo la kuwapa wanafunzi nafasi ya pili ya kuendelea na masomo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Muchaeli Ng’umbi, alisema mradi wa SEQUIP umeleta mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kuimarisha elimu ya sekondari kwa njia mbadala na kuongeza nafasi za masomo kwa wasichana.
Post A Comment: