Na Denis Chambi, Tanga.

NDEREMO na vifijo  vimetawala katika kijiji cha Kwashemshi kata ya Bungu wilayani Korogwe baada ya Serikali kutangaza  maridhiano ya pande mbili na kufikia muafaka wa kugawa hekali 100 kwaajili ya makazi ya wananchi ikiwa ni baada ya  mgogoro  uliodumu tangu miaka ya 1980 kati ya wananchi wa kijiji hicho na mwekezaji wa zao la Mkonge kampuni ya Sisal Estate.

Kwa muda mrefu asilimia kubwa ya wananchi hususani wanaume na vijana  wa kijiji hicho kila ifikapo usiku wamekuwa wakilazimika kulala nje  kwenye  uwanja wa  wanoutumia  kama soko siku za jumamosi kutokana na wengi wao kukosa makazi ya kutosha kwaajili ya  kuishi pamoja na familiya zao ambapo  zaidi ya nyumba 302 zipo ndani ya eneo la mwekezaji wa shamba la Mkonge  na ikitokea nyumba au choo  kikibomoka imekuwa ni vigumu kufanya ukarabati pasipo kuwa na kibali cha mmiliki huyo.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kwashemshi Razaro Mandia ameeleza adha hiyo ya muda mrefu ambayo wakazi wa maeneo hayo wamekuwa wakiipitia  ambapo amesema kuwa imefika hatua wamekosa matumaini na Serikali  kutokana na viongozi wengi wakiwemo mawaziri wa sekta ya ardhi ambao walifika katika eneo hilo kutafua Suluhu ya mgogoro huo lakini imeshindikana kutokana na mmiliki wa ardhi hiyo kuwa na haki kisheria ambapo wananchi wengi wa maeneo hayo walikuwa ni wafanyakazi wa Mkonge baadaye walizaliana na familiya kuongezeka.

"Ni kweli pengine Tanzania tuna uhaba wa maeneo lakini hatujafikia hatua ya wananchi kulala nje kwenye uwanja, wazazi wetu wametulea kwa hali ngumu sana katika kijiji hiki lakini inafikia hatua wazazi wa kiume na watoto wakiume wanalala nje ili wawaache wake zao na mabinti walale ndani, ikifika asubuhi  mzazi wa kiume analazimika atoke nje ili ampishe mwanae wa kike abadili nguo aende shule yote hii ni kwa sababu ardhi ya kujenga haipatikani watu wa Kwashemshi sio maskini hivyo wa kushindwa kujenga" alisema Lazaro

"Eneo hili la hapa tulipo kuna nyumba 394 kati ya hizo 94 ni za mwekezaji 92 zinaishi watu na nyingine hazitumiki , nyumba 302 ni za wananchi ila kati ya hizo hakuna yenye vyumba viwili kwaajili ya kuishi watu eneo lote tunaloishi limezungukwa na kambi ya mwekezaji wakati wote mwananchi akitaka kwenda kulima anakodishwa" alisema

Mbunge wa  Jimbo la Korogwe vijijini Timotheo Mnzava amesema kuwa  tangu miaka ya 1980 eneo la Kwashemshi limekuwa ni mkombozi wa wananchi wengi wakifanya biashara mbalimbali na kujipatia kipato kilichowawezesha kukidhi mahitaji ya familia zao  kupitia zao la Mkonge.

Mnzava ambaye pia ndiye mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge  Ardhi Malia asili na utalii amengeza kuwa kuwa Mwaka 2015 mwekezaji  alipewa mamlaka na Mahakama baada ya kushinda kesi alianza harakati za kutaka kubomoa nyumba wanazoishi wananchi hao lakini viongozi wa Serikali na chama cha Mapinduzi waliingilia kati kumuomba kuwavumilia jambo ambalo mpaka sasa wanaishi kwa huruma ya kampuni hiyo ambayo ndiyo ina hati ya umiliki wa eneo

"Eneo hili ni moja ya maeneo muhimu  tangu Miaka ya 1980 eneo hili ndio lilikuwa na soko kubwa  na lilikuwa limechangamka uchumi wake ulikuwa vizuri  kwa sababu ya kilimo cha Mkonge  uwekezaji unaofanyika una umuhimu"

"Jambo hili ni la muda na lina historia kubwa wananchi wamejenga na wanaishi ndani ya shamba la mwekezaji mwaka 2015 mwekezaji aliamua kutaka kuwatoa wananchi katika eneo hili akapeleka kesi  mahakamani akashinda na akarudi akataka kuanza kubomo nyumba za wananchi viongozi tuliingilia kati  tukafanya mazungumzo na mwekezaji Ile hali ikatulia  lakini mpaka leo hatuijui hatima ya wananchi hawa wataendelea kuvuliwa mpaka lini ikitokea mwekezaji ameondoka au kubadilisha umiliki anayekuja itakuwaje" alihoji Mnzava na kuongeza kuwa

"Wananchi hawa wamewekewa utaratibu choo kikibomoka au ukuta ukianguka kukarabati lazima apate kibali cha kampuni kwenye nchi hii inayoongozwa na Serikali ya chama cha Mapinduzi maisha hayo hatuwezi kuyafurahia hata kidogo  mwenye kauli ya mwisho katika hili ni Serikali pekee" alisisitiza Mbunge huyo.

Hatimaye waziri wa ardhi  nyumba na Maendeleo ya Makazi Deogratius Ndejembi baada ya kufanya ziara katika eneo hilo na kuzungumza na wananchi wa kijiji cha Kwa shemshi amekuja na tumaini jipya kwao baada ya kutangaza kuwa kutokana na makubaliano baina ya Serikali na mwekezaji Sisal Estate jumla ya hekali 100 za shama hilo zimemegwa   kuwagawia wananchi kwaajili ya kufanya makazi.

"January  3,2025 nilikaa na mwekezaji wa eneo hili akiwemo Mbunge , na halmashauri  tukaangalia namna bora ya kuweza kutatua mgogoro huu tayari kulikuwa na maamuzi ya muhimili mwingine ambao ni Mahakama  na ilimpa haki mwenye Estate hii sasa namna ya kuweza kutatua mgogoro huu ni lazima tutumie busara sana nikasema siwezi kuona nyumba zaidi ya 400 zinavunjwa  wakati wananchi ndio ilikiwa  kipato chao na familiya zao ambao wengi waliokuwa ni wafanyakazi wa kampuni" alisema Ndejembi.

Waziri huyo amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango na uwepo wa wawekezaji katika  maeneo mbalimbali hapa nchini akiwataka wananchi wa Kwashemshi kushirikiana katika ulinzi wa mashamba ya Mkonge ambao ni moja ya zao la kimkakati linalolimwa hapa nchini na kuitambulisha Tanzania kimataifa 

"Wawekezaji ni muhimu kwa Taifa letu uwekezaji ni muhimu na ni lazima ulindwe haya mashamba yapo ni lazima na nyinyi wananchi  mshiriki moja kwa moja katika kuyalinda ya kuyatunza mashamba hayo asije akatokea mtu na kusema eneo hilo ni la kwake baada ya kumega hekali 100"

Alisema Kamishina wa Ardhi na wataalamu walifanya tathmini ya nyumba wanazoishi wakazi wa Kwashemshi ndani ya eneo la mwekezaji na kubaini kuwa ni hekali 70 ambapo sasa Serikali imetoka na  maamuzi ya kuwapimia wananchi na kuwapa hati miliki huku hekali nyingine 30 zikirudishwa kwenye halmashauri ya mji wa Korogwe  kwaajili ya mpango bora wa matumizi ya ardhi.

"Kuanzia Leo tutakata hekali 100 kutoka kwenye shamba la estate baada ya makubaliano na kazi hiyo itaanza mara moja na Kamishina wa ardhi mkoa  lakini katika ukataji huo heka 70  zilizoingiliwa na makazi kila mmoja atarasmiahiwa na kupewa hati ya umiliki wa ardhi heka 30 tunamkabidhi Mkurugenzi azifanyie matumizi bora ya ardhi ataamua yeye na viongozi wengine watazipangia watumishi vipi"

"Kilio chenu cha muda mrefu cha kuishi kwa Mashaka kwa kuhisi labda hukumu inakuja kutekelezwa kesho sasa imekwisha  kaeni kwa amani lakini niwaombe  wananchi mlinde eneo hilo asije akajitokeza mtu kutafuta ugomvi ambao tumeshautatua heka zilizosalia baada ya kukata bado ni mali ya estate"  alisema Ndejembi.

Waziri Ndejembi ametoa maelekezo kwa Kamishna wa ardhi ndani ya  wiki mbili kufanya utambuzi wa wananchi wote wanazoishi katika eneo hilo  na zoezi la  kuwapatia hati za umiliki wa ardhi lianze  punde tu utambuzi huo utakapo kamilika.


 

Share To:

Post A Comment: