Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imetenga Shilingi Bilioni 11 kwa ajili ya Mradi wa kufunga taa kwenye Uwanja wa Ndege wa Jijini Arusha.
Hatua hiyo ya ufungaji taa za barabarani ni miongoni mwa mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita, katika kuhakikisha barabara za mijini na maeneo yote muhimu yanafungwa taa za kutosha.
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa ametoa taarifa hiyo, 08, January, 2025 baada ya kukutana na kuongea na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Christian Makonda Jijini Arusha.
Akizungumzia hatua hiyo ya Serikali, Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa, Arusha ni Mkoa muhimu kwa Utalii na uchukuzi ukiwa wa tatu kwa miruko ya Ndege nchini Tanzania, ambapo ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mkoa huo, katika kufanikisha utekelezaji wa ilani ya CCM, ikiwemo kusimamia maboresho ya Uwanja wa Ndege wa Arusha, unaotarajiwa kuanza kufungwa taa hizo hivi karibuni.
Mbali ya suala hilo, Waziri Mbarawa pia ameridhia ombi la Mkuu huyo wa Mkoa wa Arusha, la kuboresha Reli ya Kaskazini (Tanga-Arusha), katika kuboresha huduma za Utalii Mkoani humo kwa kupunguza foleni.
Katika mazungumzo yao, Makonda mbali ya kusema kuwa Sekta ya Uchukuzi ni muhimu kwenye kukuza na kuimarisha Utalii Mkoani Arusha, amesema lakini pia, kuboreshwa kwa Reli pamoja na kujengwa kwa Bandari Kavu Mkoani Arusha, kutaondoa wingi wa malori ya mizigo barabarani pamoja na kusaidia katika matunzo ya barabara katika kuzisaidia kudumu muda mrefu zaidi.
#KAZIINAONGEA
Post A Comment: