MKUU wa Mkoa wa Simiyu Mkuu Kenani Kihongosi amesema Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan amewaagiza viongozi wote kwenda kuwatumikia wananchi katika maeneo ambayo wamekabidhiwa dhamana hiyo.


Akizungumza leo Januari 9,2025 wakati anaanza ziara katika vijiji vya Nyamikoma, Mwandama, Sapiwi, Igegu Magharibi,Igegu Mashariki, Igegu, Isenge, Mwamabu, Igagalulwa, Sengerema na Majengo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Kihongosi amesema yeye yuko tayari kwenda katika vijiji kusikiliza changamoto za wananchi ili kuzipatia ufumbuzi.

“Sasa mimi niko tayari kuanzia leo kuja katika vijiji vyenu kusikiliza changamoto zinazowakabili maana kupitia nyie Wananzengo ndipo tunapoibua matatizo mbalimbali, kero zinazowakabili huku ikisaidia pia kujua wapi pana shida ikiwemo ukosefu wa huduma muhimu kama umeme, maji, afya, elimu, ukosefu wa pembejeo na hata miundombinu korofi ya barabara.”

Amesisitiza kwamba maendeleo ya watu katika mikoa, wilaya, Vijiji na hata vitongoji, yanachagizwa na viongozi kwenda katika maeneo mbalimbali kuzungumza na wananchi na kwa kuliona hilo ndio maana ameanza ziara ya siku 30 kwenda kusikiliza kero na kuzipatia ufumbuzi katika vijiji vyote vya mkoa wa Simiyu.
Share To:

Post A Comment: