Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, ameendelea na ziara yake ya kikazi akilenga kuimarisha fursa za uwekezaji katika uzalishaji wa mbegu za mazao ya kibiashara. 

Akiwa katika Kata ya Mtwango, Wilaya ya Njombe, ametembelea shamba la mkulima wa viazi mviringo na kusisitiza umuhimu wa mkoa huo kujikita katika uzalishaji wa mbegu bora za viazi mviringo.

"Tunataka Mkoa wa Njombe uwe mkoa pekee nchini kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali, ikiwa ni pamoja na zao hili la viazi mviringo, kwa sababu ardhi yetu bado ipo na tena ina rutuba. Hii itatuwezesha kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuhakikisha Tanzania inakuwa ghala la chakula barani Afrika, kama alivyoelekeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan," alisema Mhe. Mtaka.

Rais Samia, katika juhudi zake za kuifanya Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula barani Afrika, alibainisha mikakati mitatu mikuu ya serikali katika sekta ya kilimo: uwekezaji katika miundombinu ya umwagiliaji, kuboresha upatikanaji wa teknolojia na pembejeo za kisasa, na kukuza masoko ya mazao ya kilimo.

Mhe. Mtaka aliongeza kuwa Njombe inaunga mkono juhudi hizi kwa kuhakikisha inakuwa sehemu ya maghala hayo kwa kuzalisha chakula cha uhakika. Alitoa wito kwa wataalamu wa kilimo mkoani njombe kuja na mbinu mbadala za kuzalisha mbegu za mazao mbalimbali yanayolimwa Njombe, ili kuongeza uzalishaji na kipato cha wakulima.

"Upatikanaji wa mbegu bora na za uhakika utasaidia kukuza uchumi wa wananchi. Wakulima wengi wa Njombe ni wazalishaji wakubwa wa viazi mviringo, lakini wanajikuta wakipanda mbegu za asili kutokana na uhaba wa mbegu bora. Ni wakati sasa wa kuanzisha mashamba ya kuzalisha mbegu hizi ndani ya mkoa wetu ili kukidhi mahitaji ya zaidi ya tani 1,000 kwa msimu wa kilimo," alisisitiza Mhe. Mtaka.

Kwa kuzingatia ardhi yenye rutuba na hali ya hewa nzuri, Njombe ina nafasi kubwa ya kuwa kitovu cha uzalishaji wa mbegu bora za mazao mbalimbali, hivyo kuchangia katika azma ya taifa ya kuwa ghala la chakula barani Afrika.












Share To:

Post A Comment: